Dunia yaomboleza kifo cha gwiji wa muziki, Tina Turner
25 Mei 2023![USA Anaheim | Tina Turner](https://static.dw.com/image/65726591_800.webp)
Kulingana na meneja wake, Turner aliyekuwa na uraia wa Uswisi tangu mwongo mmoja uliopita, amefariki baada ya kuugua kwa muda mrefu katika makaazi yake ya Küsnacht karibu na mji wa Zurich. Wimbo wake maarufu zaidi ulikuwa "What's Love Got to Do." Mbali na kuwa malkia wa muziki, Turner alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza maarufu duniani kuzungumzia udhalilishaji wanaopitia wanawake majumbani.
Salamu za rambirambi zinaendelea kutumwa kutoka kote ulimwenguni kutoka kwa wasanii, mashabiki na hata viongozi wa nchi akiwemo Rais wa Marekani Joe Biden aliyesema kuwa Turner alikuwa na kipaji kilichobadilisha milele muziki wa Marekani.
''Juu ya kuwa na kipaji adimu kilicholeta mabadiliko ya kudumu katika muziki wa Marekani, Tina alikuwa ni mtu imara, aliyeshinda vikwazo chungu nzima, na manyanyaso, na kujenga fani itakayodumu kwa vizazi vingi na kuacha urithi ambao ni wake binafsi,'' limesema tangazo la Rais Biden kuhusiana na kifo cha Tina Turner.