1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu milioni 18 Ukanda wa Sahel kukabiliwa na baa la njaa

20 Mei 2022

UN imeonya kuwa watu milioni 18 Ukanda wa Sahel watakabiliwa na njaa kali katika muda wa miezi mitatu ijayo kutokana na athari za vita vya Urusi na Ukraine, janga la corona na mabadiliko ya tabia nchi.

Somalia | Hungersnot
Picha: Mariel Müller/DW

Baa la njaa litawashinikiza idadi kubwa ya watu kuhama kwenye maeneo yaliyoathirika, kulingana na Ofisi ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa.

Idadi kubwa ya watu katika Ukanda huo wanakabiliwa na baa la njaa tangu 2014, ambapo takribani watu milioni 17 katika nchi za  Burkina Faso, Chad, Mali na Niger wanakabiliwa na hali ya dharura ya uhaba wa chakula, kulingana na Umoja wa Mataifa.

Kote Kusini mwa Jangwa la Sahara kumekuwa na mafanikio hafifu ya shughuli za kilimo kwa zaidi ya muongo mmoja, hivyo uhaba wa chakula utaongezeka hadi mwishoni mwa msimu kiangazi, kulingana na Tomson Phiri, msemaji wa Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa.

Soma pia: Baa la njaa linanukia kutokana na kupanda bei za vyakula tangu Urusi ilipoivamia Ukraine

"Hali inazidi kuwa mbaya kabla ya kuwa nzuri zaidi,'' aliwaambia waandishi wa habari mjini Geneva. "Tunaona watu wanajaribu kuhama ili kupata riziki zao."

Watu wengi kutoka eneo hilo ni miongoni mwa wahamiaji wanaotaka kusafiri kuelekea kaskazini mwa Ulaya kwa matumaini ya fursa za kiuchumi, utulivu na usalama.

"Vurugu, ukosefu wa usalama, umaskini uliokithiri na kupanda kwa gharama za vyakula imezidisha utapiamlo na kupelekea mamilioni ya watu kwenye kiwango kibaya kabisa cha ugumu wa maisha,'' kulingana na  Martin Griffiths, mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia misaada ya kibinadamu (OCHA).

"Hivi karibuni ongezeko la bei za vyakula lililosababishwa na mzozo kati ya Urusi na Ukraine ni tishio kwa usalama wa chakula,'' alisema.

Soma pia: Wananchi wa Kusini mwa Madagascar wakaribia kutumbukia kwenye baa kubwa la njaa

Nchi hizo mbili ni ni wazalishaji wa ngano na mazao mengine ya kilimo, na mgogoro huo umepelekeaa kusitishwa uuzaji wa mazao.

Ofisi ya Griffiths imetoa dola milioni 30 kutoka kwenye mfuko wa dharura wa misaada kwa nchi nne za Afrika.

Makundi ya misaada ya kibinaadamu mapema mwaka huu yalizindua mpango wa kutafuta dola bilioni 3.8 kwa mwaka 2022, lakini wamepata chini ya asilimia 12 tu, OCHA ilisema.

  

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW