1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu milioni 8 huenda wakakosa misaada Yemen mwezi ujao

Sylvia Mwehozi
16 Februari 2022

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa takribani watu milioni 8 nchini Yemen wako hatarini kukosa misaada yote ya kiutu kufikia mwezi ujao endapo hatua za haraka hazitochukuliwa katika vita iliyodumu kwa miaka saba. 

Jemen humanitäre Hilfe verteilt
Picha: picture-alliance/AA/S. Ibicioglu

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Hans Grundberg na mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths wameelezea hali ya wasiwasi katika taifa hilo maskini la Kiarabu ambalo tayari linakabiliwa na hali tete. Wamesema mwishoni mwa mwezi Januari kulishuhudiwa karibu theluthi mbili ya mipango ya misaada ya Umoja wa Mataifa ikipunguzwa au kufungwa

Grundberg ameonya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa juu ya mashambulizi ya hivi karibuni yaliyofanywa na waasi wa Kihouthi dhidi ya Umoja wa Falme za Kiarabu na Saudi Arabia, "yanaashiria kushindwa kudhibitiwa kwa mzozo huo akitoa rai kwa pande zinazohusika kuchukua hatua za haraka kukomesha mapigano".

Ameongeza kuwa mashambulizi ya muungano wa kijeshi unaongozwa na Saudi Arabia dhidi ya vituo vya vizuizi vinavyodhibitiwa na Wahouthi huko Saada, "yalikuwa ni tukio baya zaidi la mauaji ya raia ndani ya kipindi cha miaka mitatu" na kuelezea ongezeko la kutisha la mashambulizi ya angani nchini Yemen dhidi ya makaazi ya raia mjini Sanaa na mji wa bandari wa Hodeida.

mkuu wa misaada ya kiutu wa Umoja wa Mataifa Martin Griffiths Picha: Getty Images/AFP/S. Stjernkvist

Kwa upande wake Griffiths amebainisha kwamba zaidi ya raia 650 waliuwawa au kujeruhiwa mnamo mwezi Januari katika mashambulizi ya anga, mizinga na ufyatuaji risasi wa silaha ndogo pamoja na vurugu nyinginezo, ikiwa ndio idadi ya juu ndani ya miaka mitatu iliyopita. "Vita hiyo inawakuta watu katika nyumba zao, shuleni, misikitini, hospitali na maeneo mengine ambako raia wanapaswa kulindwa".

Kulingana na Griffiths mashirika ya misaada ya Umoja wa mataifa yameishiwa fedha na kulazimika kupunguza baadhi ya programu zake. Mnamo mwezi Desemba Shirika la Mpango wa chakula duniani lilipunguza mgao wa chakula kwa watu milioni 8 na kuanzia mwezi Machi watu hao wanaweza wasipate chakula kabisa.

Yemen imekumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu mwaka 2014, wakati waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran walipochukua udhibiti wa mji mkuu wa Sanaa na karibu maeneo mengi ya kaskazini mwa nchi na kuilazimisha serikali kukimbilia eneo la Kusini kisha Saudi Arabia. Muungano wa kijeshi ukiongozwa na Saudia uliingilia vita hiyo mwaka 2015 na kuungwa mkono na Marekani, Umoja wa Falme za kiarabu ukijaribu kuirejesha madarakani serikali ya rais Abdrabbuh Mansur Mansour Hadi.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW