Watu saba wauwawa Afghanistan
25 Juni 2013Mkuu wa Jeshi la Polisi mjini Kabul, Ayoub Salangi ameliambia shirika la habari la Ujerumani DPA, wanamgambo wanne walikuwemo katika gari ambao walikuwa na vitambulisho bandia, waligunduliwa na vikosi vya usalama na waliuwawa kabla ya kutimiza lengo lao.
Nae msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afghanistan Sediq Sediqqi amesema walinzi watatu kutoka kikosi maalum cha kinachuhusika na ulinzi wa rais (PPS) wameuwawa katika purukushani za kufyatuliana risasi.
PPS ni kikosi maalumu chenye dhamana ya ulinzi wa makazi ya rais, mazingira, ofisi zilizopo ndani ya makazi hayo pamojo na ulinzi wa rais Hamid Karzai mwenyewe na familia yake.
Tayari waasi wa Taliban wamedai kuhusika na shambulio hilo kwa kusema malengo yao yalikuwa makazi ya rais, ofisi za CIA zilizopo karibu na makazi hayo pamoja na Wizara ya Ulinzi. Msemaji wa wanamgambo hao Zabihullah Mujahid amesema idadi kadhaa ya raia wa kigeni na wanajeshi wa Afghanistan wameuwawa katika shambulio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa za serikali ya Afganistan, kwa kutumia vitambulisho baandia wanamgambo hao waliweza kufika mpaka katika eneo la mbele lenye ulinzi mkali la karibu na makazi ya rais lakini hawakuweza kufikika katika jengo lenyewe.
Mmoja wa watu walioshuhudia amesema wanamgambo hao walitoka katika gari walililokuwemo wakiwa wamevaa sare za kijeshi na kuanza kuwafyatulia risasi walinzi walikuwepo katika eneo hilo. Amesema tukio hilo la kufyatuliana risasi kati ya wanamgambo na walinzi lililodumu kwa karibu masaa mawili limetokea umbali wa meta 20 kutoka katika lango kuu la kuingia katika makazi ya rais.
Takribani miripuko 16 na milio ya risasi ilisikika mapema leo na moshi mkubwa kuonekana ukifuka kutoka katika eneo la makazi ya hayo. Maafisa wa makazi hayo wamesema mapigano hayo yametokea wakati rais Karzai akiwa ndani ya makazi yake. Wanamgambo hao walikabilina vikali na walinzi wa eneo hilo pamoja na maafisa wa Marekani karibu na ofisi ya CIA kabla hawajauwawa.
Shambulio hilo limetokea muda mfupi kabla ya Karzai kufanya mkutano wake na waandishi habari. Kundi la waandishi hao pamoja na wanafunzi waliokuwepo nje ya lango hilo walilazwa chini wakati wa tukio hilo ingawa hakuna hata mmoja aliyejeruhiwa. Kiongozi huyo vilevile alipangiwa kwenda kuzindua mkutano wa kitaifa kuhusu sera ya vijana mjini Kabul, ambao baadae uliendelea pasipo uwepo wake.
Aidha shambulio hilio linatokea ikiwa imetimia wiki moja tu baada ya Taliban kufungua ofisi ya mazungumzo ya kisiasa mjini Doha, Qatar, ikiwa na lengo la kufanya majadiliano na wawikilisha wa Marekani na serikali ya Afghanistan. Wanamgambo hao wameasema wataendelea na mazungumzo sambamba na kuendeleza mapigano.
Mwandishi: Sudi Mnette DPA
Mhariri:Yusuf Saumu