1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu sita wauwawa nchini Somalia

Charo, Josephat26 Machi 2008

Mashirika ya misaada yasema Somalia ni nchi hatari

Wanamgambo wakiwa katika barabara ya mji mkuu MogadishuPicha: AP

Watu sita, wakiwemo wanajeshi wanne wa Somalia na raia wawili wameuwawa leo wakati wapiganaji wa kiislamu walipouvamia mji muhimu wa kusini wa Jowhar na kusababisha mapigano.

Maafisa wanasema wanamgambo hao wameuteka na kuudhibiti kwa muda mfupi mji wa Jowhar unaopatikana yapata kilomita 90 kaskazini mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu na kuyapekua magari na ofisi za serikali. Wapiganaji hao pia wamewakomboa wafungwa wa jela kuu mjini Jowhar na kuwaachia huru.

Serikali ya Somalia imethibitisha uvamizi huo lakini imesema wanajeshi wake wengi wamekwenda katika kijiji kilicho karibu cha El-Baraf kuichakaza kambi inayoshukiwa kutumiwa kutoa mafunzo kwa waasi.

Walioshuhudia

Mzee mmoja katika mji wa Jowhar, Mohammed Haasa Jelle, amesema wanamgambo wa kiislamu wameingia mjini humo mapema leo kupitia njia mbili tofauti na kuuteka baada ya mapigano ya muda mfupi yaliyosababisha vifo vya watu sita.

Mkaazi mwingine wa mji wa Jowhar, Said Abdullah, aliyeshuhudia uvamizi huo, amethibitisha kuwa mwanamke mmoja, mtoto wake na wanajeshi wanne wameuwawa kwenye mapigano hayo na wapiganaji wameivunja jela kuu na kuwakomboa wafungwa.

Msemaji wa wanamgambo wa kiislamu waliouvamia mji wa Jowhar, Mukhtar Robbow, amethibitisha kutekwa kwa muda kwa mji huo akiongeza kuwa wameyachukua magari kadhaa ya serikali. Amesema uvamizi huo ulilenga kuwadhihirishia wanajeshi wa Ethiopia walio nchini Somalia, na vibaraka wao yaani serikali ya Somalia, kwamba wanaweza kufanya uvamizi wakati wowote.

Afisa wa serikali ya Somalia mjini Mogadishu amesema wanajeshi walikuwa nje ya mji wa Jowhar wakati wanamgambo wa kiislamu waliouvamia. Amesema wanajeshi walikuwa wakifanya operesheni dhidi ya wanagambo katika kijiji cha El Baraf wakati wanamgambo hao walipoingia mjini Jowhar.

Mji wa Mogadishu na vitongoji vyake vimekabiliwa na machafuko ya kila siku katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita ambayo yamesbabisha vifo vya mamia ya watu na kuwalazimu maelfu ya wengine kuyakimbia makazi yao.

Wafanyabiashara wa Mogadishu wamewaajiri maafisa wa usalama wa kibinafsi kulinda mali yao katika soko la Bakara ambalo limekuwa uwanja wa mapigano kati ya makundi ya waasi yanayohasimiana.

Mashirika ya misaada

Wakati haya yakiarifiwa, mashirika 39 ya kimataifa ya kutoa misaada yanasema Somalia imekuwa hatari mno kiasi kwamba wafanyakazi wa kutoa misaada hawawezi kuwasaidia wasomali zaidi ya milioni moja wanaokabliwa na hali ngumu kutokana na athari za vita.

Malori ya shirika la mpango wa chakula la Umoja wa Mataifa WFP yakiwapelekea misaada wakaazi wa MogadishuPicha: AP

Taarifa iliyotolewa na mashirika hayo, yakiwemo Oxfam, World Vision na Save the Children, imeonya juu ya janga la kibinadamu linalokaribia kutokea nchini Somalia, huku baraza la usalama la Umoja wa Mataifa likijiandaa kukutana hapo kesho mjini New York Marekani kuijadili hali nchini Somalia.

Taarifa hiyo pia imesema mgogoro unaoikabili Somalia umeendelea kuwa mbaya kwa kasi kubwa huku idadi ya watu wanaoweza kupelekewa misaada ikizidi kupungua. Watu 360,000 wameyahama makazi yao na wengine nusu milioni wanategemea misaada ya kiutu.

Kwa wakati huu kuna watu zaidi ya milioni moja ambao wameyahama makazi yao nchini Somalia, huku machafuko ya mjini Mogadishu yakiendelea kuwalazimisha watu takriban 20,000 kuyakimbia makazi yao kila mwezi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW