1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu takriban 400 waliuliwa Congo mnamo mwezi Novemba

Saleh Mwanamilongo
6 Januari 2022

Umoja wa Mataifa umesema takriban watu 400 waliuawa kiholela nchini Congo mnamo mwezi Novemba.Uchunguzi umeonyesha kwamba asilimia 10 ya mauwaji hayo yalifanywa na vikosi vya usalama vya serikali.

Demokratische Republik Konog | Unruhen in Goma
Picha: Guerchom NdeboAFP/Getty Images

Ofisi ya Pamoja ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Kongo imesema mwezi Novemba pekee mawakala wa serikali walihusika na mauaji ya kiholela ya watu 40, wakiwemo wanaume 24, wanawake tisa na watoto saba.

Ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa jana iliongeza kuwa wapiganaji wanaomiliki silaha waliwauwa watu wasiopungua 345, wakiwemo wanawake 61 na watoto 26 katika kipindi hicho cha mwezi mmoja.

Soma pia:Watu 10 wajeruhiwa kufuatia maandamano Goma, DRC 

''Mwezi DEsemba hali ilikuwa mbaya zaidi''

Umoja wa Mataifa uliorodhesha zaidi ya visa mia nane vya ukiukaji wa haki za binadamu katika eneo lote la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, sawa na ongezeko la asilimia 61 ukilinganisha na mwezi mmoja kabla. Juhudi za kuwapata viongozi wa Kongo kutoa maoni yao, kufuatia ripoti hii hazikufua dafu.

Omar Kavota, mratibu wa shirika la kutetea haki za binadamu jimboni Kivu ya Kaskazini, CEPADHO, amesema takwimu hizo za Umoja wa Mataifa ni chini ya makadirio.

''Ripoti hii ya Umoja wa Mataifa ni yakweli.Na pengine tukizingati hali ya mambo ilivyo kwenye uwanja wa machafuko utakuta kwamba visa vya ukiukwaji wa haki za binadamu ni vingi kuliko hata Umoja wa Mataifa ulivyoripoti. Hiyo ni ripoti ya mwezi Novemba,ukitizama mwezi Desemba hali ilikuwa mbaya zaidi.'', alisema Kavota.

Soma pia:Wanamgambo 18 wauwawa Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo

Mauwaji bado yaendelea licha ya uongoza wa kijeshi

Raia waliokimbia mashambulizi ya kundi la wapiganaji wa CODECO mkoani IturiPicha: Tom Peyre-Costa/NRC

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa, visa vingi vya ukiukaji wa haki za binadamu vilifanyika jimboni Kivu ya Kaskazini, likifuatiwa na majimbo la Ituri, Tanganyika na Kivu ya Kusini. Mikoa hiyo yote iko kwenye eneo la mashariki mwa Kongo.

Tangu mwezi Mei mikoa ya Kivu Kaskazini na Ituri imekuwa chini ya uongozi wa kijeshi kwa lengo la kukomesha shughuli za makundi yenye silaha. Hatua hii ya kipekee iliyochukuliwa na Rais Felix Tshisekedi imelipa jeshi mamlaka kamili kwenye mikoa hiyo, lakini hadi sasa halijafanikiwa kuzuia mauwaji yanayofanywa na makundi yenye silaha ambayo yamevuruga eneo hilo kwa miaka 25 sasa.

Makundi ya waasi yanayohusishwa na ukatili huo ni pamoja na wapiganaji wa ADF, kundi la Nyatura, waasi wa Rwanda wa FDLR na wapiganaji wa CODECO ambao ni kundi la kikabila huko mkoani Ituri.