1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu takriban milioni 69 wameyahama makazi yao duniani

Caro Robi
19 Juni 2018

Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi UNHCR limeripoti kuwa takriban watu milioni 69 duniani wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na vita, ghasia na mateso, hiyo ikiwa idadi kubwa iliyovunja rekodi.

Bangladesch Biometrische Registrierung von Rohingya-Flüchtlinge
Picha: DW/M. Mostqfigur Rahman

 Umoja wa Mataifa umesema mamilioni ya watu katika nchi kama Myanmar na Syria wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na vita na mizozo. Kufikia mwishoni mwaka jana, idadi hiyo ilikuwa takriban milioni tatu zaidi ya ilivyokuwa mwaka 2016 na kuonesha ongezeko la asilimia 50 kutoka idadi ya watu milioni 42.7 walioachwa bila ya makazi muongo mmoja uliopita.

Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi UNHCR limesema idadi hiyo inamaanisha kati ya watu 110 duniani, mtu mmoja amelazimika kuyahama makazi yake.

UN yabaki njia panda kuhusu mzozo wakimbizi

Kamishna wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi Filippo Grandi amesema wako katika njia panda ambapo mafanikio yaliyopatikana katika kushughulikia watu waliolazimika kuyahama makazi yao duniani pia kunahitaji mtizamo mpya na wa kina ili kuhakikisha nchi na jamii zinazowahifadhi waathiriwa haziachiwi mzigo wa kutunza.

Kamishna wa Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi Filippo GrandiPicha: picture-alliance/dpa/R. Jensen

Grandi amewaambia wanahabari mjini Geneva kuwa asilimia 70 ya watu walioachwa bila ya makazi wanatokea nchi kumi, akiongeza iwapo kuna njia ya kusuluhisha mizozo katika nchi hizo kumi au angalau baadhi ya nchi hizo, basi idadi kubwa ya waathiriwa inayoshuhudiwa ikiongezeka kila mwaka, itaanza kupungua akitoa wito wa kuwepo dhima ya kisiasa kukomesha mizozo inayosababisha mamilioni ya watu kukimbilia kwingine.

Ripoti hiyo ya UNHCR inaonesha kuwa watu milioni 16.2 walikimbia kutoka makazi yao mwaka jana, wakiwemo wale waliolazimika kuyahama makazi yao kwa mara ya kwanza na wale waliolazimika kukimbia tena.

Inakadiriwa kila baada ya sekunde mbili, mtu mmoja duniani analazimika kuyahama makazi yake. Wengi wa waathiriwa hukimbia kutoka eneo moja hadi jingine nchini mwao badala ya kuwa wakimbizi katika nchi nyingine.

Kufikia mwishoni mwa mwaka jana idadi ya waathiriwa ndani ya nchi zao ilikuwa takriban milioni 40. Colombia, Syria na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zikiwa nchi zilizoshuhudia idadi kubwa mno ya waathiriwa.

Idadi nyingine ya watu milioni 25.4 walisajiliwa kuwa wakimbizi, huku nusu ya idadi hiyo wakiwa ni watoto, hicho kikiwa kiwango cha juu zaidi kuwahi kurekodiwa.

Mzozo wa Syria pekee uliwalazimisha  watu zaidi ya milioni 6.3 kuikimbia nchi, Wasyria wengine milioni 6.2 waliyahama makazi yao lakini walisalia nchini humo. Nchi ya pili iliyoshuhudia idadi kubwa ya watu kulazimika kuwa wakimbizi ni Afghanistan, ambapo watu milioni 2.6 walikimbilia kwingine kuwa wakimbizi.

Asilimia 85 ya wakimbizi hawako Ulaya na Marekani

Mzozo wa Sudan Kusini nao ulishuhudia idadi kubwa ya wakimbizi. Wakimbizi kutoka taifa hilo changa zaidi duniani iliongezeka kutoka watu milioni 1.4 mwanzoni mwa mwaka jana hadi watu milioni 2.4 ilipofika mwishoni mwa 2017.

Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Wandera

Grandi amesema Sudan Kusini inashuhudia mzozo mbaya sana unaohitaji hatua za dharura kwani serikali na wapinzani hawaonekani kutambua uzito wa mzozo huo na athari zake kwa raia wa nchi hiyo.

Wakimbizi kutoka Myanmar walifikia milioni 1.2 mwaka jana, kufuatia operesheni ya kinyama ya jeshi la nchi hiyo iliyopelekea Waislamu wa jamii ya walio wachache ya Warohingya kukimbilia nchi jirani ya Bangladesh.

Ripoti hiyo iliyotolewa leo pia imeonesha idadi kubwa ya waathiriwa nchini Iraq, Somalia na Sudan. Wapalestina milioni 5.4 bado wanaishi kama wakimbizi, huku Israel ikiadhimisha miaka 70 tangu kuundwa kwa taifa hilo lililochukua ardhi ya Wapalestina.

Na licha ya suala la uhamiaji kumulikwa Ulaya na Marekani kutokana na kuwasili kwa wahamiaji na wakimbizi katika mataifa hayo, asilimia 85 ya wakimbizi wanahifadhiwa katika nchi kama Lebanon, Pakistan na Uganda.

Uturuki ndiyo nchi inayohifadhi idadi kubwa zaidi ya wakimbizi duniani, ikiwa na wakimbizi milioni 3.5 wengi wao kutoka Syria.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Ap

Mhariri: Gakuba, Daniel