1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mogadishu: Al Shabaab yafanya mashambulizi watu 9 wauawa.

Zainab Aziz Mhariri:Tatu Karema
10 Juni 2023

Polisi nchini Somalia wamesema watu tisa wameuawa kwenye shambulio lililofanywa na wapiganaji wa kundi la Al Shabaab katika hoteli maarufu ya Pearl iliyo ufukweni jijini Mogadishu.

Somalia | Zerstörung nach Angriff auf Pearl Beach Hotel in Mogadishu
Picha: Farah Abdi Warsameh/AP/picture alliance

Kundi hilo la Al shabaab limekiri kuhusika na shambulio hilo kwenye hotel maarufu ya Pearl katika fukwe za mji mkuu wa Somalia, Mogadishu siku ya Ijumaa.

Miongoni mwa waliouawa katika hoteli hiyo maarufu ínayoitwa Pearl, ni raia sita na askari watatu, polisi wameeleza  katika taarifa yao.

Lido Beach, hoteli maarufu iliyo katika ufukwe wa pwani ya Somalia.Picha: Mohamed Odowa/dpa/picture alliance

Mkurugenzi wa kampuni ya huduma ya magari ya wagonjwa ya Aamin,  Abdikadir Abdirahman, amesema maafisa wake waliwabeba watu wapato 20 waliojeruhiwa kutoka kwenye eneo la tukio.

Polisi imesema vikosi vya usalama viliwaokoa raia 84 na mpaka sasa hatima ya washambuliaji waliohusika na shambulio hilo bado haijulikani.

Shirika la Habari la Kitaifa la Somalia limeandika kwenye ukurasa wake Twitter kwamba vikosi vya usalama vilifanikiwa kuwadhibiti wapiganaji wa al Shabaab waliohusika na shambulio la kigaidi kwenye hoteli hiyo maarufu ya Pearl iliyopo kwenye ufukwe wa bahari mjini Mogadishu.

Siku ya Jumamosi, uchafu ulionekana kutapakaa kwenye hoteli hiyo kutokana na shambulio lililotokea na vilionekana vioo vya madirisha vilivyovunjika pamoja na damu.

Uharibifu uliofanyika katika hoteli ya Pearl mjini Mogadishu.Picha: Farah Abdi Warsameh/AP/picture alliance

Hussein Mohamed, mhudumu anayefanya kazi katika hoteli nyingine iliyo karibu, amesema alisikia mlipuko uliofuatiwa na milio ya risasi wakati mashambulizi yalipoanza.

Soma:Somalia: Al-Shabaab yakamata kambi ya jeshi ya Janay Abdale

Kundi la Al-Shabaab lenye mafungamano na kundi la kigaidi la Al Qaeda limesema ndiyo limehusika na shambulio hilo, limeeleza wapiganaji wake walifanikiwa kuingia katika hoteli ya Pearl kupitia kwenye ufukwe.

Mnamo Novemba mwaka uliopita kundi hilo ambalo linadhibiti baadhi ya maeneo ya nchi ya Somalia, wapiganaji wake waliishambulia hoteli nyingine maarufu ya Lido iliyo pia kwenye ufukwe wa bahari mjini Mogadishu, na kusababisha vifo vya watu tisa.

Awali Al Shabaab walidhibiti eneo kubwa la Somalia kabla ya kushindwa nguvu na kurudishwa nyuma katika operesheni zinazoendeshwa na vikosi vya serikali tangu mwaka jana. Lakini wanamgambo hao bado wana uwezo wa kufanya mashambulizi dhidi ya sehemu muhimu za serikali, za kibiashara na hata za kijeshi.

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Al Shabaab.Picha: picture alliance / AP Photo

Soma:Uganda yathibitisha kupoteza wanajeshi shambulio Somalia

Mwishoni mwa mwezi Mei, wapiganaji wa Al Shabaab walishambulia kambi ya kijeshi ya Bulo Marer waliyokuwepo wanajeshi wa Uganda wa kulinda amani wa kikosi cha Umoja wa Afrika. Wanajeshi 54 waliuawa kwenye shambulio hilo liliofanyika umbali wa kilomita 130 kusini magharibi mwa jiji la Mogadishu.

Vyanzo: RTRE/AFP