1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wa Ethiopia kupiga kura katika uchaguzi mkuu Jumatatu

Zainab Aziz Mhariri: John Juma
20 Juni 2021

Bodi ya taifa ya uchaguzi nchini Ethiopia imesema uchaguzi muhimu utafanyika kesho Jumatatu na imeahidi kwamba uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki katika taifa hilo la pili barani Afrika lenye idadi kubwa ya watu.

Äthiopien | Wahlen

Msemaji wa bodi hiyo Solyana Shimeles ameliambia shirika la habari la AFP kwamba anao uhakika juu ya kufanyika kwa uchaguzi huo baada ya kukabiliwa na changamoto kadhaa.

Hata hivyo uchaguzi hautafanyika kwenye humusi moja ya majimbo 547 kutokana na ghasia na changamoto za miundombinu. Watu katika maeneo hayo watapiga kura mnamo mwezi wa Septemba lakini hakuna mipango juu ya kufanyika uchaguzi kwenye jimbo la Tigray. Jimbo hilo la watu milioni sita lilikumbwa na mgogoro wa kivita hivi karibuni.

Picha: Ben Curtis/AP Photo/picture alliance

Kwenye baadhi ya maeneo, zoezi la kupiga kura litahujumiwa kutokana na wapinzani kuususia uchaguzi. Msemaji wa bodi ya uchaguzi ameeleza kuwa ni vyama vitatu tu ambavyo havikuruhusiwa kushiriki kati ya vyama 49 vilivyosajiliwa. Amesema wajumbe 9,500 watashiriki katika kinyang'anyiro hicho kwenye ngazi za kitaifa na majimbo.

Soma Zaidi:Hali ya wanasiasa wa Ethiopia yazidi kudorora magerezani

Idadi hiyo ni kubwa kuliko zote zilizoshuhudiwa katika chaguzi zilizopita nchini Ethiopia. Hata hivyo katika jimbo la Waziri Mkuu Abiy Ahmed lenye watu wengi kuliko jimbo lingine lolote, mjumbe ni mmoja tu atakayeshiriki katika uchaguzi huo.

Kwa upande wake msemaji wa kamati ya kitaifa ya uchaguzi Solyana Shimeles amehakikisha kwamba zoezi la Jumatatu litakuwa bora zaidi, kutokana na ushiriki wa wote aidha amesema zoezi hilo litakuwa la haki.

Kamati hiyo ya uchaguzi ilifanyiwa ukarabati baada ya Waziri Mkuu Ahmed kuingia madarakani mnamo mwaka 2018, katika mukdhata wa harakati za kuipinga serikali na kuazimia kuufungua uwanja wa siasa baada ya miaka mingi ya uwatala wa mabavu.

Picha: Yohannes Gebireegziabher/DW

Waziri mkuu Ahmed alimteua Birtun Mideska aliyekuwa jaji wa ngazi ya juu hapo awali kuwa mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi. Mideska ambaye ni kiongozi wa upinzani alikuwa kwenye hifadhi ya kisiasa nje ya nchi. Uteuzi wake ulizingatiwa kuwa ushahidi wa msimamo wa dhati wa Waziri Mkuu Abiy Ahmed wa kuleta mageuzi ya kidemokrasia nchini Ethiopia.

Soma Zaidi:Umoja wa Mataifa wasikitishwa na mzozo wa Tigray

Uchaguzi wa kesho utasimamiwa na waangalizi kutoka nchi tano pamoja na maalfu ya wajumbe wa asasi za kiraia. Tume ya kitaifa ya haki za binadamu iliyochunguza tuhuma za kukiukwa haki za binadamu imenyimwa ruhusa ya kusimamia uchaguzi.

Wakati huo huo serikali ya Ethiopia imekaza nati za taratibu za vibali vya kuingia nchini. Wizara ya mambo ya ndani imesema utaratibu wa kutoa vibali vya kieletroniki na vingine mara tu mtu anapoingia nchini Ethiopia umesimamishwa kwa muda.

Vyanzo:/AFP/DPA

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW