1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSenegal

Senegal: Maandamano ya kupinga kuahirishwa uchaguzi

5 Februari 2024

Polisi nchini Senegal imetumia mabomu ya machozi kuwasambaratisha siku ya Jumapili waandamanaji katika mji mkuu Dakar.

Senegal Dakar 2024 | Waandamanaji wakipinga hatua ya kuahirisha uchaguzi
Waandamanaji wakijaribu kukimbia baada ya Polisi kuwatawanya mjini Dakar: 04.02.2024Picha: Zohra Bensemra/REUTERS

Waandamanaji walimiminika barabarani kupinga uamuzi wa Rais Macky Sall wa kuahirisha kwa muda usiojulikana uchaguzi mkuu uliokuwa umepangwa kufanyika Februari 25 mwaka huu.

Miongoni mwa waliokamatwa wakati maandamano hayo ni pamoja na Waziri Mkuu wa zamani Aminata Touré na Anta Babacar Ngom, mmoja wa wagombea urais katika uchaguzi huo.

Polisi wa Senegal wakijiandaa kukabiliana na waandamanaji wanaopinga uamuzi wa Rais Macky Sall wa kuahirisha uchaguzi: 04.02.2024Picha: Seyllou/AFP/Getty Images

Wakati wabunge wa shirikisho wakijiandaa kujadili mswada utakaopitisha uamuzi huo wa rais Sall, viongozi wa upinzani walitoa wito kwa wananchi kutetea demokrasia huku kukiwa pia na shinikizo la kuwepo kwa mazungumzo na jumuiya ya kikanda ya Afrika Magharibi, ECOWAS.

Soma pia:Mgombea wa urais na kiongozi wa upinzani nchini senegal akataliwa maombi yake ya kuwania urais 

Serikali ilisitisha matangazo ya televisheni ya kibinafsi ya Walf iliyokuwa ikipeperusha maandamano hayo moja kwa moja. Kamati ya kimataifa ya kuwalinda wanahabari imelaani hatua hiyo ya serikali na kutoa wito kwa mamlaka za Senegal kuhakikisha kwamba "Waandishi wa habari wanafanya kazi yao bila vizuizi."

Umoja wa Ulaya wataka uchaguzi wa Senegal ufanyike

Ofisi ya Kamisheni ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, UbelgijiPicha: Kenzo Tribouillard/AFP/Getty Images

Umoja wa Ulaya umetoa wito kwa wahusika wote nchini Senegal kushirikiana pamoja kwa ajili ya kuandaa uchaguzi wa haki na uwazi, jumuishi na wa kuaminika haraka iwezekanavyo.

Msemaji wa Umoja wa Ulaya ambaye pia anahusika na Sera ya Mambo ya Nje na Usalama Nabila Massrali ametoa tamko hilo siku ya Jumapili saa chache kabla ya kuanza kwa maandamano hayo ya upinzani mjini Dakar.

Msemaji huyo wa Umoja wa Ulaya amesema kuahirishwa kwa  uchaguzi wa rais nchini Senegal  kunaanzisha nyakati za mashaka nchini humo.

 Uamuzi wa Rais wa Senegal kuahirisha uchaguzi huo

Rais Macky Sall wa Senegal alipokuwa akitangaza uamuzi wa kuahirisha uchaguzi mkuu: 03.02.2024Picha: RTS/Reuters

Rais Macky Sall wa Senegal alitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi uliopangwa kufanyika Februari 25 kwa muda usiojulikana, kwa kile alichokitaja kuwa ni kuanzishwa kwa uchunguzi dhidi ya madai ya rushwa miongoni mwa wagombea.

Soma pia: Ousmane Sonko afutwa kwenye orodha ya kugombea urais nchini Senegal

Rais Sall ambaye muhula wake unafikia mwisho Aprili 2, 2024, hakutoa tarehe maalum ya uchaguzi lakini akasema majadiliano ya kitaifa yatafanyika ili kuhakikisha  uchaguzi unakuwa huru, wa wazi na shirikishi.

Wachambuzi wanasema mzozo wa Senegal unaliweka mashakani taifa hilo lenye demokrasia imara hasa kutokana na nchi za ukanda huo kukumbwa na matukio ya mapinduzi ya serikali.

Senegal imeingia kwenye mzozo kufuatia mivutano ya kisiasa yenye vurugu baada ya wagombea wa upinzani kunyimwa haki ya kushiriki uchaguzi huo ambao sasa umeahirishwa kwa muda usiojulikana.

 

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW