Watu waanza kurejea mjini Goma baada ya Volkano kutulia
23 Mei 2021Mamia ya raia waliokimbilia nchini jirani ya Rwanda wameonekana wakirudi majumbani wengi wakisema wamekabiliwa na uhaba mkubwa wa vyakula.
Miongoni mwa hao ni wale waliopoteza nyumba zao kutokana na tope la Volkano na wameirai serikali ya DRC kuwapatia msaada wa haraka.
Wakati hali ikianza kurejea na kuwa ya kawaida, idara inayoshughulikia milima ya moto pamoja na maafisa wa Baraza la Usalama jimboni Kivu ya Kaskazini wametangaza kuwa watu wasiopungua 9 wamepoteza maisha kwenye mkasa huo.
Wengi ya waliofariki ni watoto, walemavu na watu walioshindwa kukimbia baada ya tope la moto wa Volkano lilipoyafikia maeneo ya jirani la mlima Nyiragongo.
Wataalamu wawatahadharisha waathirika dhidi ya kurejea kwenye makaazi mapema
Afisa mkuu wa shirika la uchunguzi wa milima ya moto hapa Goma Muhindo Adalbert amesema bado ni mapema sana kwa watu kurejea kwenye makaazi yao akionya hatari bado ni kubwa katika muda wa saa chache zinazokuja.
Wakati huo huo, kiongozi makamu wa Shirika la Kimataifa linaloyashughulikia msaada wa kiutu nchini Congo, UNOCHA, Diego Zorrila amesema wamejitayarisha kuwahudumia waathirika wa janga hilo la tope la Volkano kutoka mlima Nyiragongo katika saa zijazo.
Hadi kufikia sasa wakaazi wanaoishi katika nyumba za ghorofa wameamua kubaki nje hasa wakati huu ambapo bado matetemeko ya ardhi yanaendela kuutikisa mji wa Goma.
Ama kuhusu wale waliokimbilia upande wa Rwanda, serikali ya mjini Kigali imesema iliwapokea watu elfu 10 lakini sasa idadi iliyobaki haizidi watu mia moja.
Idadi ya waliokimbilia Rwanda yazidi kupungua
Upande wa serikali ya Rwanda viongozi wanasema wakimbizi waliopokelewa ni takribani elfu 10 lakini kwa sasa
Mkaazi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Maria amemwambia mwandishi habari wa DW mjini Kigali kuwa "Tuliona kule kwenye Volkano moto unawaka sana... tulikimbia na njiani hatukupata tatizo, tukafika mpakani mwa Rwanda, kweli walitupokea vizuri na tukavuka salama"
Gavana wa Mkoa wa Magharibi upande wa Rwanda François Habitegeko ambao ndio unapakana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo ameieleza DW jinsi Rwanda ilivyowashughulikia wakimbizi hao.
Afisa huyo amesema "Pamoja na kwamba walikuja kwa kushtukiza tuliwapokea vizuri na kuwahakikishia usalama hakuna aliyedhurika."
Mipaka ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ilikuwa imefungwa tangu mwaka jana katika juhudi za kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona. Wakimbizi walipofika ilibidi mipaka ifunguliwe ambapo walipokelewa na kupelekwa uwanja wa mpira wa Rubavu huku wengine wakihifadhiwa mashuleni ambapo wanasema wameshughulikiwa kwa ukarimu.
Mara ya mwisho mlipuko kutokea katika Mlima Nyiragongo ilikuwa mwaka 2002 ambapo watu zaidi ya 100 walipoteza maisha huku wengine wakikimbilia nchini Rwanda kuyanusuru maisha yao.