JamiiPapua New Guinea
Watu wahamishwa kutoka maeneo hatari Papua New Guinea
28 Mei 2024Matangazo
Afisa wa serikali wa mkoa wa Enga kulikotokea mkasa huo, Sandis Tsaka, ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, wanafanya kila wawezalo kuwahamisha watu na kwamba sehemu hiyo ni kama "bomu linalosubiri kuripuka."
Afisa huyo ameeleza kuwa idadi ya watu wanaokadiriwa kuathirika na janga hilo ni takriban 7,900.
Mapema siku ya Ijumaa, watu waliokuwa wakiishi sehemu za milimani katika mkoa wa Enga nusra waangamizwe wote baada ya kutokea maporomoko ya udongo katika Mlima Mungalo.
Kituo cha kitaifa kinachoshughulikia majanga kinahofia kuwa zaidi ya watu 2,000 wamezikwa wakiwa hai japo miili ya watu watano tu na mguu wa mwathirika mmoja ndio imetolewa kutoka kwenye udongo hadi sasa.