271011 Sacharow-Preis
14 Desemba 2011Miji mikuu ya mataifa ya Kiarabu imekuwa ikijikuta inakumbwa na wimbi la mageuzi ya Kiarabu. Vuguvugu la umma linaziangusha tawala za muda mrefu za kidikteta au angalau kuzilazimisha kubadilika. Kutoka maandamano yaliyoanzishwa na watu wachache, hadi kugeuka kuwa ya maelfu, na hadi kuwa vita nchini Libya, Yemen na sasa Syria, nyuma yake kuna watu wa kawaida tu, ambao ndio waliobeba dhima kubwa ya kulisawiri vuguvugu lenyewe.
Wakati Rais wa Bunge la Ulaya, Jerzy Buzek, alipotangaza washindi wa nishani hii mwezi Oktoba 2011, sauti yake ilibeba hamasa ya hali ya juu. Alisema kwamba Bunge hilo liliamua kutoa tuzo ya mwaka huu ya Sakharov kwa ajili ya uhuru kwa wawakilishi watano wa wimbi la mageuzi ya Kiarabu, akimtaja shahidi Mohammed Bouazizi kutoka Tunisia, msichana Asma Mahfouz kuroka Misri, mzee Ahmed al-Subair Ahmed al-Sanussi kutoka Libya na mwanasheria Rasan Saituneh na mchora vikatuni Ali Farsat kutoka Syria.
Muuza mboga wa Kitunisia, Mohamed Bouazizi, alikuwa na miaka 26 tu mwaka jana, pale polisi ya nchi hiyo ilipomchukulia mkokoteni wake na kumdhalilisha, kitendo ambacho kilimsababisha kuchukuwa maamuzi ya kujiripua kwa mafuta huku akipiga mayowe: "Mwisho wa umasikini, mwisho wa kukosa ajira!"
Wiki mbili baadaye alifariki akiuguza majeraha hospitalini. Lakini kitendo chake cha kujichoma kwa moto, kikaibua maandamano Tunisia nzima, ambayo nayo yakauinuwa ulimwengu mzima wa Kiarabu.
Tarehe 18 Januari 2012, msichana mmoja alikaa mbele ya kamera yake mjini Cairo, na kujirikodi mwenyewe kuelezea kutoridhika kwake na utawala wa Misri na kuwashajiisha watazamaji wake, akisema: "Mimi ninasema hapana kwa ufisadi. Ninasema hapana kwa utawala huu."
Huyo alikuwa ni Asma Mahfouz, mwanamke wa miaka 26. Aliituma video hiyo kwenye mtandao wa Facebook, ikiwa na ombi lililosomeka: "Njoo kwenye uwanja wa Tahrir na tuunge mkono. Pigania haki yako. Maelfu ya Wamisri wakaitikia wito huo wa kupigania uhuru wao. Dhamira yao ilikuwa kuwepo kwa usawa wa kijamii, haki za msingi na mageuzi ya kidemokrasia. Leo hii Asma Mahfouz ana marafiki 13, 818 katika mtandao wa Facebook.
Bunge la Ulaya pia limemtambua raia wa Libya, Ahmed al-Zubair Ahmed al-Sanusi, mzee wa miaka 77, aliyekuwa mfungwa wa kisiasa. Kwa muda wa miaka 31 aliselelea kwenye jela za utawala wa Gaddafi, wakati mwingi akiwa amefungwa minyororo peke yake.
Hivi leo al-Sanusi amerudi kuwa miongoni mwa wanasiasa walioongoza na kufanikisha uasi dhidi ya Gaddafi. Mwisho wa wiki hii alizungumzia namna miaka 42 ya udikteta wa Gaddafi ilivyokuwa na namna vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miezi kadhaa vilivyoendeshwa.
Nchini Syria wanaharakati wawili wanaendelea kupambana na kusubiri jaala yao. Kwa miezi kadhaa sasa, mwanasheria wa haki za binaadamu, Razan Zaitouneh, anaishi kwa kujificha. Blogu yake, 'Syrian Human Rights Information Link', inatoa ripoti za uvunjwaji wa haki za binaadamu unaofanywa na vikosi vya serikali na watu wanaopotea. Anapigania kumpeleka Rais Bashar al-Assad katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.
Moyo huo huo ndio alionao mchora vikatuni, Ali Farzat. Akiakisi hisia na matakwa ya waandamanaji, michoro yake kila siku imekuwa inatoa ujumbe wa moja kwa moja. Assad naye hajamwacha hivi hivi, bali Farzat amejikuta akilipa gharama kubwa pia. Vyombo vya habari vya kigeni vilimuonesha Farzat amelazwa hospitali akiwa na majeraha kichwani na mikono yake imevunjwa. Sababu ni kuwa alichora kikatuni kinachomuonesha Assad amesimama na mzigo wake njiani anasimamisha gari kumuomba lifti Muammar Gaddafi amchukuwe naye safarini.
Kupitia maandamano ya miezi kadhaa, Asma Mahfouz alipoteza marafiki zake. Ndio maana ameiambia Idhaa ya Kiarabu ya Deustche Welle kwamba nishani hii si yake peke yake.
"Tuzo hii inanitambua mimi kama msichana jasiri. Lakini hapana, Wamisri wengi ni majasiri kuliko mimi. Wao ndio wanaostahi kuitwa hivyo. Nina fahari kwamba mimi ni mmoja kati yao na kwamba naishi katika nchi hii." Amesema Asma.
Mwandishi: Stefanie Duckstein
Tafsiri: Mohammed Khelef
Mhariri: Othman Miraji