1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaKenya

Watu wanne wafariki kufuatia maporomoko ya udongo Kenya

Michael Kwena9 Aprili 2024

Watu wanne kutoka jimbo la Narok nchini Kenya wamefariki kufuatia maporomoko ya udongo. Hii inafuatia mvua kubwa zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali za taifa hilo la Afrika mashariki.

mvua yasababisha maafa makubwa Kenya
Watu wanne wa familia moja kutoka Kijiji cha Torokiat mjini Narok wamefariki baada ya nyumba yao kuporomokewa na udongoPicha: REUTERS

Kwa wiki ya tatu sasa,mvua kubwa zimekuwa zikishuhudiwa sehemu mbalimbali ya taifa huku uharibifu mkubwa ukiendelea kuripotiwa.

Jimbo la Narok limekuwa la hivi punde kuripoti hasara kutokana na mvua. Watu wanne wa familia moja kutoka Kijiji cha Torokiat wamefariki baada ya nyumba yao kuporomokewa na udongo.

Mvua hizo kadhalika zimesababisha mamlaka ya kitaifa inayosimamia barabara nchini KeNHA ,kufunga baadhi ya barabara za humu nchini ikiwemo ile ya North Horr kuelekea Kalacha baada ya mafuriko kuharibu barabara hiyo.

Mvua yasababisha maafa zaidi Kenya

Katika jimbo la Kisumu,angalau familia mia tatu kutoka eneo bunge la Nyando zimeachwa bila makazi kufuatia mvua hizo. Wakaazi wakiilalamikia serikali ya kaunti hiyo kwa kushindwa kushughulikia  tatizo la mafuriko kila mara mvua inaponyesha.

Nairobi pia imeathirika kwa mvua hiyo kubwa

Mvua kubwa yasababisha hasara kubwa ya mali pamoja na vifo nchini Kenya Picha: REUTERS

Jimbo la Nairobi pia limekuwa likishuhudia mvua kubwa,wakaazi wakimtaka Gavana wa Nairobi Johnson Sakaja kuwajibika. Wanailaumu serikali ya kaunti hiyo kwa kushindwa kujenga mabomba ya kupitisha maji ambayo ndiyo chanzo cha mafuriko katika mitaa mbalimbali.

Hayo yakijiri,basi la abiria lililokuwa likitoka Garissa kuelekea Nairobi lilisombwa na mafuriko katika Daraja la Areli japo abiria wote waliondoka bila majeraha. Kamanda wa Polisi wa jimbo la Tana River Ali Ndiema amethibitisha kuwa,juhudi za uokozi zinaendelea.

Ikumbukwe, idara ya utabiri wa hali ya anga,imetangaza kuendelea kushuhudiwa kwa mvua kubwa haswa maeneo ya pwani,kati na magharibi mwa kenya kwa wiki hii. Hadi sasa,hakuna takwimu iliyotolewa na serikali au shirika la msalaba mwekundu kuhusu idadi kamili ya maafa kutokana na mvua ya sasa.

Michael Kwena, DW Marsabit

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW