1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Watu wanne washitakiwa kwa shambulizi la Moscow

25 Machi 2024

Watu wanne wanaotuhumiwa kwa kufanya shambulizi lililotokea kwenye ukumbi wa tamasha nchini Urusi ambalo liliwauwa zaidi ya watu 130 wamefikishwa mahakamani mjini Moscow.

Waombolezaji waliweka mauwa nje ya Ukimbi wa Tamasha wa Crocus City Hall
Urusi inaomboleza vifo vya zaidi ya watu 130 waliouawa katika shambulizi la tamasha la muziki MoscowPicha: Vitaly Smolnikov/AP Photo/picture alliance

Washukiwa hao walionesha dalili za kupigwa wakati walifunguliwa mashitaka ya ugaidi. Mmoja alionekana kabisa kutokuwa na fahamu wakati wa kikao cha kusikilizwa kesi yao.

Soma pia: Washirika wa Urusi wamtaka Putin kufikiria kurejesha kifo kwa magaidi na wauaji

Taarifa ya mahakama ilisema wawili kati ya washukiwa hao walikiri kuhusika na shambulizi hilo baada ya kushitakiwa katika kikao cha awali cha kusikilizwa kesi, ingawa hali ya watu hao ilizusha maswali kuhusu iwapo walikuwa wakizungumza kwa uhuru.

Mahakama ya Wilaya ya Basmanny mjini Moscow iliwashtaki rasmi Dalerzdzhon Mirzoyev mwenye umri wa miaka 32, Saidakrami Rachabalizoda, 30, Shamsidin Fariduni, 25, na Mukhammadsobir Faizov, 19 kwa kufanya shambulizi la kigaidi la kikundi lililosababisha vifo vya wengine.

Soma pia: Urusi yafanya maombolezo ya kitaifa

Shitaka hilo lina adhabu ya juu ya kifungo cha maisha jela. Mahakama hiyo iliamuru kuwa watu hao wote, ambao ni raia wa Tajikistan, wawekwe kizuizini hadi Mei 22. Rais wa Urusi Vladmir Putin ameapa kulipiza kisasi kwa waliohusika na shambulizi hilo la kikatili.