Watu wapatao 11 wauwawa kwenye vurugu nchini Kenya
12 Agosti 2017Hali ya wasiwasi bado imetanda katika maeneo ya mabanda ya Kibera na Mathare jijini Nairobi. Hadi kufikia sasa watu kumi na moja wameuawa katika vurugu hizo. Kulingana na taarifa ya polisi, miili ya watu hao waliouawa kwa kupigwa risasi tayari imeshapelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Jijini Nairobi. Miongoni mwa watu waliouwawa wakati wa makabiliano makali kati ya polisi na waandamaji ni msichana mmoja mdogo.
Makabailiano na waandamanaji
Polisi walikabiliwa na kibarua kigumu na kulazimika kutumia risasi na vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wameziba barabara huku wakichoma matairi wakijaribu kutumia njia hii kuonyesha ghadhabu zao. Maafisa wa polisi wamewakamata watu kadhaa kufuatia ghasia hizo.
Kaimu waziri wa mambo ya ndani na usalama wa taifa Fred Matiang'i amesema baadhi ya majangili wameitumia hali hii ili kuendeleza uhalifu na uporaji wa mali za watu. Matiang'i pia amelaani kitendo cha kutuma ujumbe wenye maneno ya kuchochea chuki katika mitandao ya kijamii.
Hali mjini Kisumu
Katika mji wa Kisumu ulio magharibi mwa Kenya wafuasi wa kiongozi wa upinzani Raila Odinga walifanya vurugu usiku wa kuamkia Jumamosi kwa kile walichokiita kuwa kiongozi wao ameibiwa kura.
Kwa mujibu wa taarifa ya polisi, watu wawili waliuwawa kwa kupigwa risasi katika vurugu ambazo zilianza muda mfupi baada ya rais Uhuru Kenyatta kutangazwa kuwa ni mshindi.
Daktari Ojwang Lusi mganga mkuu katika kaunti ya Kisumu magharibi ameeleza kuwa watu wengine wanne wamelazwa hospitalini kutokana na kupata majeraha baada ya kupigwa risasi. Na habari kutoka mji wa Siaya ulio kusini magharibi mwa Kenya zinaarifu juu ya polisi kushindwa kuuchukua mwili wa mtu aliyepigwa risasi kutokana na waandamanaji kuwazuia kuuchukua mwili huo.
Wakati huo huo viongozi wa kidini wametoa wito kwa Wakenya wa kudumisha amani na wamewataka maafisa wa usalama kutotumia nguvu wanapokabiliana na waandamanaji. Sehemu nyingi ni tulivu katika nchi ya Kenya ambayo ina watu zaidi ya milioni 40.
Mwandishi: Zainab Aziz/APE/RTRE
Mhariri: Sylvia Mwehozi