Watu waruhusiwa kutembea nje kwa mara ya kwanza Uhispania
3 Mei 2020Wakati huo huo baadhi ya mataifa ya Ulaya kwa tahadhari yalilegeza vizuwizi vya kutoka nje, wakati Urusi na Ujerumani zimeripoti ongezeko la maambukizi. Wakati serikali zikitafakari kuondoa vizuwizi vya kuwataka wananchi kubakia majumbani ili kuanzisha tena uchumi wao, maafisa nchini Marekani wameleta matumaini kiasi kwa kuidhinisha dawa ya majaribio ili itumike kwa wagonjwa wa ugonjwa wa COVID-19.
Uamuzi huo ulikuwa wa hivi karibuni kabisa katika hatua za dunia kutafuta dawa na chanjo kwa ajili ya virusi vya corona, ambavyo vimesababisha nusu ya binadamu dunia kuwamo katika vizuwizi vya kutoka nje na kuuweka uchumi wa dunia kuelekea katika mporomoka mbaya kabisa tangu mdororo mkuu katika miaka ya 1930. Virusi sasa vimewauwa zaidi ya watu 242,000 duniani kote, kwa mujibu wa idadi iliyowekwa pamoja na shirika la habari la AFP, na walioambukizwa wanafikia milioni 3.4 tangu kuzuka mara ya kwanza virusi hivyo nchini China mwishoni mwa mwaka jana.
Kukiwa na ishara kwamba janga hili linapungua kasi katika mataifa yale yaliyoathirika zaidi , mataifa ya Ulaya pamoja na baadhi ya sehemu za Marekani yameanza kuondoa vizuwizi kujaribu kurejesha hali ya maisha kuwa ya kawaida katika uchumi ambao ulioathirika kutokana na wiki kadhaa za kufungwa.
Watu watembea mitaani
Kuanzia Madrid hadi Mallorca, Wahispania walimiminika mitaani baada ya kuruhusiwa kufanya mazowezi na kutembea huru nje baada ya serikali kulegeza wiki saba za udhibiti mkubwa wa kuwataka wananchi wake kubakia majumbani katika nchi hiyo iliyokuwa na moja ya idadi ya juu kabisa ya vifo vilivyofikia zaidi ya 25,000. "Baada ya wiki kadhaa za kufungiwa, nilikuwa nahitaji sana kutembea nje, kukimbia, na kuona dunia," alisema mshauri wa masuala ya fedha Marcos Abeytua mjini Madrid. "Jana nilikuwa kama mtoto katika mkesha wa krismass."
Uhispania, Ujerumani, Austria na mataifa ya Scandinavia taratibu yanalegeza vikwazo vya kuwazuwia watu kutoka majumbani, wakati kesi za virusi vya corona zikipungua licha ya kuwa hatua za watu kukaa mbali mbali zitaendelea, matumizi ya barakoa pamoja na uchunguzi kujaribu kufuatilia maambukizi.
Ufaransa, ambayo itaondoa sehemu ya vizuwizi vya kutotembea nje hapo Mei 11, jana Jumamosi (02.05.2020) ilirefusha hali ya dharura ya kiafya kwa miezi miwili zaidi hadi mwishoni mwa Julai wakati ikiripoti vifo vipya 166, ikiwa ni idadi ya chini kabisa ya vifo katika zaidi ya wiki tano.
Idadi ya kesi zilizothibitishwa za virusi vya corona nchini Ujerumani imeongezeka kwa watu 793 na kufikia 162,496, ikiwa ni data kutoka taasisi ya kupambana na magonjwa ya kuambukiza ya Robert Koch RKI , leo Jumapili (03.05.2020).
Idadi ya vifo vilivyoripotiwa imepanda kwa watu 74 na kufikia vifo 6,649 kwa jumla.