1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wasiopungua 20 wameuawa jimboni Kivu ya Kusini

28 Desemba 2021

Duru kutoka Kivu ya Kusini zasema watu wasiopungua 20 wamepoteza maisha wakati wa mapambano makali yanayoripotiwa mtaani Fizi baina ya waasi na jeshi.

Kongo Bijombo | Soldaten | South Kivu Provinz
Picha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Mashuhuda mbalimbali wanaeleza kwamba mapigano yanaendelea kati ya jeshi la FARDC na muungano huo wa wanamgambo wa Gumino na Twigwaneho wakiongozwa na kanali aliyeasi jeshi la Congo akidai kutetea maslahi ya kabila lake la Banyammulenge, Michel Rukundo Makanika, katika vijiji vya Kamombo, Nyamara na Chakira katika nyanda za wilaya ya Fizi. Jeshi limepoteza udhibiti wa vijiji hivyo ambayo kwa sasa viko chini ya udhibiti wa wanamgambo.

Msemaji wa operesheni ya kijeshi inayoitwa Sokola ya Pili katika eneo la kusini mwa mkoa wa Kivu Kusini, Meja Dieudonné Kasereka anasema kwamba jeshi la Congo limejiondoa katika maeneo hayo kisha kushambuliwa kwa sababu za kimkakati ili kuepusha uharibifu na maafa zaidi kama vile vifo vya raia.

Je, wanajeshi wa Burundi wako Kivu kusini?

Wakaazi wa Fizi wanaendelea kukimbia maendeo yao kufuatia mapigano baina ya jeshi na waasi wa Gumino na TwigwanehoPicha: Alexis Huguet/AFP/Getty Images

Shambulizi hilo linafanyika muda mfupi baada ya wakaazi wa Bonde la Mto Ruzizi ndani ya wilaya jirani ya Uvira wakisema wameshuhudia kuna askari wenye silaha nzito nzito waliovuuka Mto Ruzizi tangu wiki moja upande wa Kitemesho wakidai wanatokea Burundi, na kujielekeza katika Milima ya Lemera na Bwegera. Ila msemaji huyo wa jeshi la Congo hajathibitisha uwepo wa jeshi la Burundi kwenye ardhi ya Congo.

''Sina taarifa hiyo, lakini kumekuwa na ushirikiano baina ya makundi ya wapiganaji ya Congo na yale ya Burundi'',alisema Meja Dieudonné Kasereka,msemaji wa jeshi jimboni Kivu ya Kusini.

Mgomo baridi mjini Bukavu

Wakati huo huo, shughuli nyingi zinazorota tangu asubuhi mjini Bukavu kufuatia wito wa asasi za kiraia katika mkoa wa Kivu Kusini zilizotangaza siku hii kuwa bila kazi kwenye eneo lote la mkoa huo ili kuonesha mshikamano na wakaazi wa mkoa jirani wa Kivu ya Kaskazini wanaokuwa wahanga wa ukosefu wa usalama kila leo, na pia kupinga kile zinachohisi kuwa mipango ya kuigawa Congo kwa tishio la kuingia kwa askari na polisi wa kigeni kwenye ardhi ya Congo. 

Masoko, maduka, benki, havijafungua milango, isipokuwa tu magari na pikipiki zinazo tumika. Katika tangazo moja, serikali ya mkoa wa Kivu Kusini imepinga wito huo wa asasi za kiraia ikisema kuwa haioni umuhimu wa siku hii bila kazi, ikialika pia wakazi kufanya shughuli zao kama kawaida. Serikali ya Congo imehakikisha kwamba licha ya changamoto, juhudi za kurejesha amani mashariki ya Congo zinaendelea kufanyika.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW