1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu watano wakamatwa Chad kufuatia maandamano

17 Mei 2022

Watu watano wamekamatwa nchini Chad kufuatia maandamano dhidi ya Ufaransa, ambapo waandamanaji wanatuhumiwa kuunga mkono utawala wa kijeshi nchi hiyo, vyanzo vya upinzani na polisi vilisema Jumatatu.

Tschad N'Djamena | Demonstration von Anhängern der NGO Wakit-Tama
Picha: Blaise Daruistone/DW

Max Loalngar, msemaji wa kundi la upinzani la Wakit Tamma lililoitisha maandamano hayo, alithibitisha kuwa watu watano wamekamatwa.

Vituo saba vya mafuta ya kampuni  ya Ufaransa,Total  vilishambuliwa, ambapo polisi walijeruhiwa katika machafuko hayo yaliyotokea  Jumamosi katika mji mkuu N'Djamena, kulingana na afisa wa polisi ambaye alizungumza kwa sharti la kutotajwa jina.

"Viongozi watano wa maandamano" wamekamatwa, "na wanazuiliwa katika makao makuu ya idara ya usalama wa ndani," chanzo kilisema.

Nchi za Magharibi zilikubali unyakuzi

Chad imekuwa chini ya utawala wa kijeshi tangu rais wake Idriss Deby Itno alietawala kwa miaka 30 alipouawa Aprili 2021 wakati wa operesheni za kuwaangamiza waasi kaskazini mwa nchi hiyo, na mtoto wake  Mahamat Idriss Deby Itno, ambaye ni jenerali, alinyakua madaraka.      

wanajeshi wa Ufaransa wakiwa kwenye operesheni ChadPicha: Philippe De Poulpiquet/MAXPPP/dpa/picture alliance

Unyakuzi huo ulikubaliwa na nchi za Magharibi, zikiongozwa na Ufaransa ambayo ni mkoloni wa zamani wa nchi hiyo, ambayo inaiona Chad kama mshirika wa karibu katika mapambano yake dhidi ya wanajihadi katika Sahel.

Hivi karibuni kumekuwa na mapinduzi  barani Afrika ikiwemo nchini Guinea, Mali na Burkina Faso na  yamekabiliwa na vikwazo vya kikanda.

Kulingana na Loalngar, "hawahusiki na vitendo vya uharibifu. Wamekamatwa kimakosa," alisema."Polisi waliwaondoa katika eneo kuu la  maandamano, kisha maandamano ya hapa na pale  yakatokea  baadaye sisi hatuhusiki," alisema.

Wanafunzi nao waandamana

Vyama kadhaa vya upinzani vimetoa wito wa kuachiliwa kwa waliokamatwa.

Shirika la habari la AFP lilisema mamia walishiriki maandamano hayo na  bendera mbili za Ufaransa zimechomwa moto.

Mahamat Idriss Deby wakati wa mazishi ya babake Picha: Christopeh Petit Tesson/AFP/Getty Images

Siku ya Jumatatu, maandamano yaliofanywa na  mamia ya wanafunzi wa shule ya upili, wengi wao wakiimba kuwa  "wafaransa waondoke," yalitawanywa na polisi huko N'Djamena, AFP ilishuhudia.

Hakukuwa na mtu aliyekamatwa au kujeruhiwa, afisa wa polisi aliiambia AFP. Mwishoni mwa juma, waziri wa mawasiliano Abderamane Koullamallah alilaani ghasia hizo.

Utawala wa kijeshi ulitangaza baada ya kuchukua mamlaka kwamba utafanya "uchaguzi huru na wa kidemokrasia" ndani ya miezi 18 baada ya kuandaa kongamano la kitaifa kuhusu matatizo ya Chad.

Hata hivyo, "mazungumzo yake ya upatanisho wa kitaifa" ambayo yalikuwa yameanza Mei 10 yameahirishwa.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW