1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu watatu wapona virusi vya Corona nchini Congo

23 Aprili 2020

Wakati visa vingi vya maambukizi ya virusi vya Corona vikiripotiwa katika mji wa Kinshasa, Mkoa wa Kivu ya Kaskazini, umeshuhudia kupona kwa wagonjwa watatu katika miji ya Beni na Goma.

Coronavirus Afrika Nigeria Lagos Essensausgabe
Picha: Reuters/T. Ade

Ni mgonjwa mmoja tu ambaye amebaki hospitalini akisubiri matokeo ya vipimo vya mwisho ili naye pia arudi nyumbani.

Kupona kwa wagonjwa wa Virusi vya Corona katika mkoa huu, kumewapa furaha baadhi ya wakaazi wa miji pamoja na wilaya za mkoa wa Kivu ya Kaskazini kwani,kuripuka kwa ugonnjwa huo katika mkoa huu, kumewaathiri wakaazi wengi, wanaoishi kwa kutegemea vibarua.

Akiwahutubia wakaazi wake katika kituo wanakotibiwa wagonjwa wa covid 19 katika mji wa Beni, Meya wa mji huu Bwanakawa Mass Nyonyi alianza kuwashukuru na kuwapongeza wagonjwa waliokubali kubaki hospitalini kwa kipindi kisichopungua mwezi mmoja, na hasa kwa uvumilivu wao, pale akiwajulisha kwamba, wakaazi wote wa Beni walikuwa wanawaombea.

Na akiwa mwenye furaha, mgonjwa mmoja  mwanamama aliyepona, alimshukuru Mungu kwa kumponya, huku akiwahimiza ndugu na dada zake kuwa waangalifu, na kuheshimu kanuni zinazotangazwa na madaktari, ili kujikinga dhidi ya homa hatari inayosababishwa na virusi vya Corona.

Marufuku ya usafiri kati ya miji ya Butembo na Goma yaondolewa

Picha: picture-alliance/AP Photo/T. Hadebe

Kuondoka hospitalini kwa wagonjwa wa virusi vya Corona waliopona, kumemfanya gavana wa mkoa wa Kivu ya Kaskazini Carly Kasivita, kuondoa marufuku ya safari kati ya miji ya Butembo na Goma, mukiwemo wilaya za Walikale, Masisi pamoja na Rusthuru.

Mji wa Beni kaskazini mwa mkoa huu, pamoja na mji mdogo wa Bunagana ulioko kaskazini magharibi, ndiyo imetengwa na maeneo mengine kwani, bado kuna mgonjwa mmoja wa Corona mjini Beni, wakati Bunagana kuna kisa kinachoshukiwa kuwa cha Corona.

Hatua ya kupigwa marufuku kwa safari za abiria katika mkoa wa Kivu ya Kaskazini, imeshayaathiri maisha ya wakaazi wengi wa miji ya Beni na Butembo, miji hiyo ikiwa inategemeana kwa vyakula na bidhaa mbalimbali.

Ikiwa mgonjwa wa Beni ataondoka hospilini leo, wakaazi wa Beni wataruhusiwa tena kusafiri kutoka mji huu kwenda miji mingine kama ilivyokuwa kabla ya mlipuko wa virusi vya corona.

Chanzo: John Kanyunyu DW Beni


 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW