Watu watatu wauawa katika maandamano ya kuipinga Taliban
18 Agosti 2021Video zilizochukuliwa na kituo cha habari cha Pajhwok Afghan News, zimeonyesha waandamanaji waliokuwa wamebeba bendera ya Afghanistan wakikimbia, huku milio ya risasi ikisikika.
Watu kadhaa walikusanyika katika mji wa mashariki wa Jalalabad kuipandisha bendera ya Afghanistan, siku moja tu kabla ya maadhimisho ya uhuru wa Afghanistan. Watu hao waliishusha bendera ya Taliban, nyeupe na yenye maandishi ya Kiislamu, ambayo wanamgambo hao wamekuwa wakiipandisha katika maeneo waliyoyakamata kama ishara ya kuonyesha utawala wao.
Soma zaidi: Ndege za kijeshi zarejelea safari zake Kabul
Afisa wa zamani wa polisi ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa watu wanne wameuawa na wengine 13 wamejeruhiwa katika maandamano hayo, bila ya kutoa maelezo zaidi.
Hata hivyo Reuters haikuweza kuthibitisha jinsi vifo hivyo vilivyotokea na pia msemaji wa Taliban hakupatikana alipotafutwa kutoa tamko juu ya tukio hilo.
Naye Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson ameonya kuwa Taliban inapaswa kuhukumiwa kwa vitendo vyake na wala sio kwa maneno na ahadi wanazozitoa.
UAE yampa hifadhi Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani
Akilihutubia bunge la Uingereza, Johnson pia ametetea jinsi serikali ya Uingereza ilivyoshughulikia mgogoro wa Afghanistan akisisitiza kuwa nchi hiyo haingeweza kuendelea kubakia Afghanistan bila ya msaada wa Marekani.
"Tutakuja na mpango salama na wa kisheria kwa Waafghan walio na uhitaji mkubwa na walio hatarini kuja kuishi hapa Uingereza. Kando na wale Waafghani ambao wamefanya kazi na sisi. Natangaza leo kuwa tunajitolea kuwahamisha Waafghani wengine 5,000 mwaka huu, na mpango mpya utazingatia wale walioko hatarini hasa wanawake na watoto na tutaendelea kuangalia hali hii kwa lengo la kuwapa hifadhi Waafghani hadi 20,000 katika miaka ijayo."
Baada ya mazungumzo wiki hii na viongozi wengine wa mataifa ya Magharibi akiwemo Rais Joe Biden wa Marekani, Johnson amesema viongozi hao kwa sauti moja wamekubaliana kuwa litakuwa kosa kwa nchi yoyote kuitambua serikali mpya ya Afghanistan kabla ya kuzingatia vitendo vyao juu ya haki za binadamu, haki za wasichana kupata elimu, ugaidi, uhalifu na kupambana na dawa za kulevya.
Soma zaidi: Safari za ndege zafungwa Afghanistan
Wakati hayo yakiarifiwa, Waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za kiarabu amesema Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani yuko nchini humo baada ya kuikimbia nchi hiyo.
Kupitia taarifa, wizara hiyo imesema Umoja wa Falme za kiarabu umempa hifadhi Rais Ghani pamoja na familia yake kutokana na sababu za kibinadamu.