1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu 3 wauawa na 66 kujeruhiwa katika maandamano Msumbiji

8 Novemba 2024

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema leo kuwa watu wapatao 30 wameuawa nchini Msumbiji katika takriban wiki tatu za msako dhidi ya waandamanaji.

Waandamanaji mjini Maputo
Waandamanaji mjini MaputoPicha: Amós Fernando/DW

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch (HRW) limesema leo kuwa watu wapatao 30 wameuawa nchini Msumbiji katika takriban wiki tatu za msako dhidi ya waandamanajibaada ya uchaguzi wa Oktoba 9 uliokumbwa na utata.

HRW imeliambia shirika la habari la AFP kwamba watu hao waliuawa kati ya Oktoba 19 na Novemba 6, idadi ambayo haijajumuisha vurugu zilizorekodiwa Novemba 7 wakati maafisa wa polisi na wanajeshi walipowatawanya maelfu ya waandamanaji katika mji mkuu wa nchi hiyo, Maputo.

Haya yanajiri huku hospitali kuu nchini Msumbiji ikisema leo kuwa takriban watu watatu waliuawa na wengine 66 kujeruhiwa wakati wa makabiliano kati ya polisi na waandamanaji hapo jana kutokana na uchaguzi uliokumbwa na utata.

Dino Lopes, mkurugenzi wa huduma ya dharura kwa watu wazima katika hospitali hiyo kuu ya Maputo, amewaambia waandishi wa habari kwamba kati ya majeruhi hao 66, 57 inawezekana walijeruhiwa kwa silaha,wanne walianguka, watatu kupigwa na wawili walijeruhiwa kwa silaha zenye ncha kali.

Lopes ameongeza kuwa wengi wa waathiriwa hao walikuwa kati ya umri wa miaka 25 na 35 huku wengine wakiwa na umri wa chini ya miaka 15.