1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wengine 2 wauawa katika maandamano Sudan

14 Januari 2022

Watu wawili wameuwawa katika maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi nchini Sudan.

Sudan Proteste
Picha: AFP/Getty Images

Muandamanaji mmoja na polisi mmoja waliripotiwa kuuawa jana wakati vikosi vya usalama vikivunja kwa nguvu maandamano ya kupinga utawala wa kijeshi, na kuongeza idadi ya waliouawa kutokana na maandamano hayo yaliyoanza Oktoba kufikia hadi angalau watu 64.

soma Sudan: Waziri mkuu Abdalla Hamdok ajiuzulu

Vifo hivyo vinajiri siku chache baada ya Umoja wa Mataifa kutoa wito wa kukomeshwa kwa ghasia dhidi ya waandamanaji na kusema kuwa vitawezesha mazungumzo ya kitaifa kutatua mzozo wa kisiasa nchini humo.

soma Kujiuzulu kwa Hamdok huenda kukarejesha staili ya uongozi wa Bashir

Polisi adungwa visu

Abdel Fattah al-BurhanPicha: Mahmoud Hjaj/AA/picture alliance

Kamati Kuu ya Madaktari wa Sudan (CCSD), ambayo inaambatana na vuguvugu la maandamano, ilisema "shahidi mmoja" alikufa baada ya kupigwa risasi tumboni tarehe 13 Januari.

Wizara ya mambo ya ndani ilishutumu wale iliyowataja kama "watu wasiotii" kwa kumuua afisa mkuu wa polisi wakati wa maandamano katika mji mkuu, Khartoum.

soma Marekani yahimiza utawala wa kiraia baada ya Hamdok kujiuzulu

Wizara hiyo ilisema polisi huyo "alidungwa kisu mara kwa kadhaa katika sehemu mbalimbali za mwili wake alipokuwa akitekeleza jukumu lake la kuwalinda waandamanaji".

Shirika la habari la serikali la Suna liliripoti kwamba mtawala wa kijeshi Luteni Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alihudhuria mazishi ya polisi huyo jana jioni. 

Polisi watumia nguvu kupita kiasi

Picha: Mahmoud Hjaj/Anadolu Agency/picture alliance

Tovuti ya habari inayoungwa mkono na upinzani ya Al-Rakoba iliripoti kwamba kwa mara ya kwanza, mamlaka za usalama hazikutekeleza hatua zozote kali za kawaida ambazo ni pamoja na kufungwa kwa madaraja na kusitishwa kwa mawasiliano na huduma za mtandao.

soma Maelfu waandamana Sudan kupinga utawala wa kijeshi

Makundi yanayounga mkono demokrasia yamekuwa yakifanya maandamano ya mara kwa mara ili kudai utawala kamili wa kiraia.

Al-Rakoba imeripoti kwamba muungano wa madaktari wa Sudan umevishutumu vikosi vya usalama vya nchi hiyo kwa kutumia nguvu kupita kiasi  katika kukabiliana na waandamanaji katika maandamano ya hapo jana.

Kamati Kuu ya Madaktari ya Sudan ilisema katika taarifa yake kwenye mitandao ya kijamii kwamba "vikosi vya mamlaka ya kikatili vilishiriki katika ukiukaji wa mbaya wa haki za binaadam katika kuvunja maandamano ya Alhamisi kwa kutumia risasi za moto na aina zote za ukandamizaji".

Chama cha Wanataaluma wa Sudan ambalo ni kundi lilihamasisha maandamano dhidi ya Rais wa zamani Omar al-Bashir mwaka 2018 na 2019 lilisema kulikuwa na hitaji kubwa la madaktari wa upasuaji na timu za matibabu katika Hospitali inayomilikiwa na serikali ya Bahari, huko Khartoum Kaskazini.

Chama hicho kimesema kulikuwa na majeruhi wengi  wenye majeraha ya risasi za moto lakini haikutoa takwimu maalum.

Jeshi la nchi hiyo ndilo lenye mamlaka kamili baada ya Waziri Mkuu Abdalla Hamdok kujiuzulu tarehe 2 Januari. Hamdok alihudumu kama waziri mkuu tangu 2019 kabla ya kukamatwa na jeshi mnamo Oktoba na baadaye kurejeshwa tena katika wadfa huo mwezi mmoja baadaye.