1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wenye matatizo ya akili duniani wanaishi kifungoni

7 Oktoba 2020

Ripoti ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch imesema mamia ya watu wenye matatizo za afya za akili kote ulimwenguni wanakabiliwa na vifungo.

Indonesien Java Psychiatrie Patienten Fixierung
Picha: HRW/Andrea Star Reese

Wanaume kwa wanawake na watoto, miongoni mwao wenye umri mdogo wa hadi miaka 10 hufungiwa kwenye vyumba vidogo kwa wiki, miezi ama hata miaka. 

Kulingana na ripoti hiyo ya Human Rights Watch, haya yanafanyika kwenye mataifa angalau 60 huko Asia, Afrika, Ulaya, Mashariki ya Kati na hata Amerika.

Ripoti hiyo ya kurasa 56 iliyopewa jina "Kuishi na minyororo: Vifungo vya watu wanaoishi na matatizo ya kiakili ulimwenguni”, inaangazia namna gani watu hao wanavyokabiliwa na vifungo vya mara kwa mara majumbani ama kuzingirwa na uchafu kinyume na ambavyo wangetamani kuishi kutokana na kuongezeka kwa unyanyapaa na kukosa huduma za maradhi hayo.

Matatizo ya akili na changamoto zilizoko?

This browser does not support the audio element.

Wengi hulazimika kula, kulala, kujisaidia haja ndogo na hata kubwa kwenye chumba hicho hicho kidogo wanachoishi. Na hata kwenye vituo vya huduma za afya vya serikali ama binafsi pamoja na vile vya kidini ama vya kienyeji, mara nyingi wagonjwa hawa hulazimishwa kukaa bila kula, kunywa dawa za kienyeji na zaidi kunyanyaswa kingono.

Ripoti hii inajumuisha tafiti zilizofanywa kwenye maeneo kadha wa kadha pamoja na shuhuda kutoka Afghanistan, Burkina Faso, Cambodia, China, Ghana, Indonesia, Kenya, Liberia, Mexico, Msumbiji, Nigeria, Sierra Leone, Palestina, jimbo lililojitangazia uhuru la Somaliland, Sudan Kusini, na Yemen.

Mgonjwa wa afya ya akili Picha: picture alliance/empics/D. Lipinski

Mtafiti mwandamizi wa shirika hilo, anayeangazia haki za wenye ulemavu Kriti Sharma anasema udhalimu huo uko dhahiri kwenye jamii nyingi. Watu hao hufungiwa mara kwa mara kwenye miti ama vibandani kwa sababu familia hupambana kukabiliana na hali hiyo huku serikali zikishindwa kutoa huduma zinazohitajika.

Human Rights Watch liliwahoji zaidi ya watu 350 wenye matatizo ya akili miongoni mwao watoto, familia za watu 430, watumishi wa vituo vya wagonjwa hao, wataalamu wa magonjwa ya afya ya akili, wanaoponya kwa imani, maafisa wa serikali na wapigania haki za watu wa aina hiyo.Soma Ukosefu wa Mazoezi wachangia matatizo ya kiafya

Ulimwenguni kote, inakadiriwa watu milioni 762 ama 1 kati ya 10 ikiwa ni pamoja na Watoto 1 kati ya 5 wana matatizo ya afya za akili. Lakini hata hivyo, serikali zinatumia chini ya asilimia 2 ya bajeti zao za afya kuwatibu wagonjwa hao.

Pamoja na kukosekana huduma, ukosefu wa ufahamu pia ni changamoto. Familia nyingi zinahisi kama hazina chaguo lengine zaidi ya kuwafunga ndugu zao. Mara nyingi wanahofia kwamba wanaweza kukimbia ama kujiumiza wenyewe.

Familia ambazo hasa huwafungia wagonjwa ni zile zinazoamini maradhi hayo husababishwa na ushirikina ama kutenda dhambi na ndio maana huwapeleka kwa waganga wa kienyeji ama kuombewa na ikishindikana ndio hukimbilia hospitali. Mura, mzee wa miaka 56 anayeishi Bali Indonesia, aliombewa na waponyaji na waombezi wa kidini 103 na iliposhindikana, alifungiwa.

Sharma anahitimisha kwa kusema, inatisha kwamba maelfu ya watu ulimwenguni wanaishi wakiwa wamefungwa minyororo, kudhulumiwa na kutengwa.

HRW

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW