1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu wenye silaha wavamia gereza Nigeria, wawaachia wafungwa

13 Septemba 2021

Watu wenye silaha za kivita wamelivamia gereza moja katikati mwa Nigeria na kuwaachia huru wafungwa kadhaa. Huku hayo yakijiri, wanafunzi waliotekwa nyara mwanzoni mwa mwezi huu kwenye Jimbo la Zamfara, wameachiwa huru.

Nigeria I Überfall auf Gefängnis
Picha: David Dosunmu/AP/picture alliance

Msemaji wa gereza la Kabba, kwenye jimbo la Kogi, Francis Enobore amesema kuwa gereza hilo lilivamiwa na watu wenye silaha ambao bado hawajajulikana na kuwaachia huru wafungwa 240. Enobore amesema washambuliaji kadhaa walishiriki katika mapambano ya kurushiana risasi na walinzi wenye silaha wa gereza hilo majira ya usiku wa Jumapili.

Ameongeza kusema kuwa hata hivyo, watu hao wenye silaha walilivamia gereza lililokuwa na wafungwa 294 kwa wakati huo, wakiwemo mahabusu 224 ambao kesi zao bado zinasikilizwa. Gereza hilo lilianzishwa mwaka 2008 na lina uwezo wa kuchukua wafungwa 200. Matukio ya kuvunjwa kwa magereza makubwa sio ya kawaida nchini Nigeria.

Vikosi vya Nigeria vinazidiwa nguvu na wapiganaji

Katika shambulizi la Aprili 5, watu wenye silaha walivamia makao makuu ya polisi wa Owerri na kuwaachia huru zaidi ya mahabusu 1,800. Imeelezwa kuwa mara nginyi vikosi vya usalama vya Nigeria vinazidiwa nguvu na kukabiliwa na uasi wa wapiganaji wa jihadi uliodumu kwa miaka 12 kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa Enobore, Mkaguzi Mkuu wa Magereza nchini Nigeria, Haliru Nababa ameanzisha upelelezi kuhusu shambulizi hilo na ameamuru wafungwa waliotoroka watafutwe. Ametoa wito kwa umma kwa ujumla kutoa ushirikiano wa taarifa zitakazosaidia kukamatwa tena kwa wafungwa waliotoroka.

​​Wanafunzi wa shule ya Salihu Tanko, Bosso Nigeria waliachiwa huru na watekajiPicha: AP/picture alliance

Wakati huo huo, wasichana 75 waliotekwa nyara kwenye shule moja ya sekondari katika Jimbo la Zamfara wameachiwa huru. Gavana wa jimbo hilo, Bello Matawalle amesema wanafunzi hao waliotekwa nyara tarehe moja ya mwezi huu wa Septemba katika kijiji cha Kaya, jana usiku waliungana na familia zao.

''Leo nina furaha sana kuona juhudi tunazozifanya zinafanikiwa. Kuona kwamba tumeweza kulitafutia ufumbuzi tatizo hili linalotuathiri,'' alisema Matawalle.

Msaada wa baadhi ya watekaji

Matawalle amesema polisi walifanikiwa kuwaokoa wanafunzi hao kwa msaada wa baadhi ya watekaji nyara ambao walisalimu amri na kujutia kile walichokifanya.

Utekaji huo ulisababisha shule za msingi na sekondari za serikali kwenye Jimbo la Zamfara kufungwa. Zaidi ya wanafunzi 1,100 wametekwa nyara tangu mwezi Desemba mwaka uliopita. Polisi imesema wametekwa nyara na magenge ya majambazi yenye silaha kwa lengo la kulipwa pesa ili waweze kuwaachia huru. Hata hivyo, msemaji wa gavana wa Jimbo la Zamfara amesema hakuna pesa zozote zilizolipwa kwa wanafunzi hao 75 kuachiwa huru.

Ama kwa upande mwingine vyombo kadhaa vya Nigeria tangu jana usiku vinaripoti kuwa watu waliokuwa na silaha wameivamia kambi ya jeshi kwenye Jimbo la Zamfara na kuwaua wanajeshi 12. Hata hivyo, alipotakiwa kutoa maoni yake, msemaji wa Jeshi, Meja Jenerali Benjamin Sawyer hajakanusha wala kuthibitisha taarifa hizo.

(AFP, AP, Reuters)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW