Watu wote 157 wafariki katika ajali ya ndege ya Ethiopia
10 Machi 2019Hakuna mtu hata mmoja aliyenusurika kati ya watu 157 waliokuwa kwenye ndege ya shirika la ndege la Ethiopia iliyoanguka jumapili asubuhi (10.03.2019) ikitokea mji mkuu wa Ethiopia Adis Ababa kuelekea Nairobi Kenya,kwa mujibu wa shirika la habari la Ethiopia. Raia kutoka mataifa 33 walikuwemo kwenye ndege hiyo yenye nambari ya usajili ET 302 iliyoanguka karibu na mji wa Bishoftu ulioko kiasi kilomita 50 Kusini Mashariki mwa mji mkuu Adis Ababa kwa mujibu wa ripoti.
Msemaji wa shirika la ndege ya Ethiopia ameliambia shirika la habari la kijerumani Dpa, raia 32 wakenya, Waethiopia 17, na wachina 8 ni miongoni mwa abiria waliokufa waliokuwa wakisafiri na ndege hiyo. Hakuna taarifa za haraka zilizotolewa kuthibitisha uraia wa abiria wengine waliokuwemo kwenye ndege hiyo.
Ndege aina ya Boeing 737 iliyokuwa na abiria 149 na wafanyakazi 8 iliruka mwendo wa saa 8.38 za asubuhi kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bole na kupoteza mawasiliano dakika chache baadae kwa mujibu wa shirika hilo la ndege la Ethiopia.
Ofisi ya waziri mkuu wa Ethiopia kwa niaba ya serikali imetowa ujumbe wa salamu za rambirambi kwa familia za waliopoteza wapendwa wao katika ajali hiyo. Shughuli ya utafutaji miili na uokoaji zinaendelea ingawa imeelezwa hakuna mtu aliyenusurika huku pia ikitajwa kwamba chanzo kilichosababisha ajali hiyo hakijafahamika.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Sylvia Mwehozi