Watu zaidi wauawa kwenye mashambulizi ya jeshi la Israel
24 Septemba 2025
Shirika la ulinzi wa raia kwenye Ukanda wa Gaza limesema makumi ya Wapalestina wameuawa kutokana na mashambulizi ya wanajeshi wa Israel hii leo Jumatano, huku jeshi likiendeleza mashambulizi zaidi katika mji wa Gaza City ambapo maelfu ya watu wamelazimika kuukimbia mji huo.
Majeshi ya Israel yanaendelea kusonga mbele kuingia katikati ya Jiji la Gaza City hali inayozidi kuhatarisha maisha ya Wapalestina ambao walikuwa wanaweka matumaini kwamba kwamba kuongezeka kwa shinikizo dhidi ya Israel juu ya kusitisha mapigano huenda ingesadia kunusurika kupoteza makazi yao.
Rais wa Marekani Donald Trump alikutana na viongozi wa nchi za Kiislamu katika Umoja wa Mataifa mjini New York siku ya Jumanne, kwa mazungumzo ambayo yaliyolenga usitishaji wa kudumu wa vita, kuachiliwa kwa mateka wa Israel na kuutatua mgogoro wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.
Wakati huo huo Waziri wa Ulinzi wa Italia Guido Crosetto, amesema nchi yake imepeleka meli ya kikosi cha wanamaji kuzisaidia boti za misaada zinazoelekea Gaza baada ya waandaaji wa msafara huo kusema boti zao kadhaa zililengwa na ndege zisizo na rubani pembezoni mwa Bahari ya Ugiriki.
Wanaharakati katika boti ya Global Sumud moja wapo kati ya boti zilizo kwenye msururu vyombo vya baharini vilivyosheheni misaada Flotilla wamesema zaidi ya milipuko kumi na mbili ilisikika karibu na boti yao ilipokuwa ikisafiri kutoka Ugiriki jioni ya jana Jumanne, naumefanyika uharibifu uliosababishwa na vitu visivyotambulika vilivyoanguka kwenye boti hiyo.
Umoja wa Mataifa umetoa mwito wa kufanyika uchunguzi huru kuhusu madai ya "mashambulizi" ya ndege zisizo na rubani dhidi ya boti za misaada zinaloelekea Gaza Msemaji wa Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa Thameen Al-Kheetan amesema katika taarifa ya ofisi hiyo ya Haki kwamba yeyote anayehusika na "ukiukaji" huo anapaswa kuwajibishwa kisheria.
Wakati huo huo walinda amani wa Umoja wa Mataifa wamesema ndege isiyo na rubani ya Israeliimedondoka kwenye makao yao makuu lakini haikusababisha hasara yoyote.
Kikosi hicho kinachojulikana kama UNIFIL, kimesema kuruka ndege za Israel zisizo na rubani juu ya anga ya Lebanon ni kitendo kinbachokiuka azimio la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1701 lililowezesha kuvimaliza vita vya miezi 14 kati ya Israel na Hezbollah mnamo mwaka 2006.
UNIFIL imesema wataalam wake waliidhibiti droni hiyo mara ilipoanguka kwenye makao makuu kwenye mji wa mpakani wa Lebanon wa Naqoura. Kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa cha kulinda amani kimesema ndege hiyo isiyo na rubani haikuwa na silaha bali ilikuwa na kamera. Kwa mujibu wa taarifa, jeshi la Israel baadaye lilithibitisha kuwa droni hiyo ilikuwa yao.
Vyanzo: AFP/AP/RTRE