Watu zaidi ya 120 wafariki kufuatia tetemeko la ardhi Tibet
7 Januari 2025Kiongozi wa kiroho wa eneo la Tibet ametaja kuhuzunishwa mno na tetemeko la ardhi lililotokea hivi leo, huku rais wa Urusi Vladimir Putin akimtumia salamu za pole mwenzake wa China Xi Jinping kufuatia janga hilo lililosababisha vifo vya zaidi ya watu 100.
Kiongozi huyo kiroho wa Tibet anayefahamika kwa jina la Dalai Lama amesema pia kuwa anawaombea wale wote waliofariki pamoja na majeruhi wa tetemeko hilo kubwa la ardhi.
Katika taarifa yake, Dalai Lama ambaye yuko uhamishoni ametaja kuhuzunishwa sana na janga hilo lililosababisha vifo vya watu wengi, majeraha na uharibifu mkubwa wa nyumba na mali. Amesema maombi yake yanaelekezwa kwa wale ambao wamepoteza maisha huku akiwatakia ahueni ya haraka wale wote waliojeruhiwa.
Dalai Lama alikuwa na umri wa miaka 23 tu alipoutoroka mji mkuu wa Tibet - Lhasa kwa kuhofia maisha yake baada ya wanajeshi wa China kuzima uasi wa mwaka 1959. Alivuka milima ya Himalaya yenye theluji hadi nchini India, na kiongozi huyo wa kiroho mwenye umri wa miaka 89 sasa na anayeamini mfumo wa kidini unaotokana na mafundisho ya Siddharta Gautama anayejulikana kama Buddha hajawahi kurejea tena Tibet.
Dalai Lama, ambaye sasa ana umri wa miaka 89, alijiuzulu kama mkuu wa kisiasa mwaka 2011, na kuachia mamlaka kwa serikali iliyochaguliwa kidemokrasia na baadhi ya Watibeti 130,000 kote duniani.
Soma pia: Wabunge wa Marekani wakutana na Dalai Lama
Kiongozi wa serikali hiyo iliyo uhamishoni Penpa Tsering ametoa ufafanuzi kuhusu tetemeko hilo lililopiga eneo la China lenye mamlaka ya ndani la Tibet.
"Hili ni tetemeko la sita kwa ukubwa kutokea katika eneo hilo katika kipindi cha miaka 100 iliyopita. Lilishuhudiwa mwendo wa saa tatu na dakika tano asubuhi karibu kabisa na mpaka wa India katika eneo linaloitwa Tingri. Watu kati ya 65 na 95 wamekufa kama ilivyoripotiwa saa chache zilizopita na wengine 130 wamejeruhiwa."
Idadi ya vifo yaongezeka na Urusi yatuma salamu za rambirambi
Taarifa za hivi punde kutoka vyombo vya habari vya serikali ya China zinaeleza kuwa idadi ya vifo imeongezeka hadi kufikia watu 126.
Rais wa Urusi Vladimir Putin amemtumia salamu za rambirambi mwenzake wa China Xi Jinping kutokana na tetemeko hilo la ardhi lililotokea Tibet na kusema Urusi inajumuika na wale waliopoteza ndugu na jamaa kutokana na janga hili la asili.
Tetemeko hilo lilikuwa na ukubwa wa 6.8 kwenye kipimo cha Richter lakini shirika la utafiti wa Jiolojia la Marekani limesema lilikuwa kubwa zaidi hadi kipimo cha 7.1. Maafisa wa eneo hilo wamesema zoezi la uokoaji bado linaendelea kwa kuwa na kwamba kuna uwezekano watu wengine wengi bado wamenaswa chini ya vifusi.
(Vyanzo: AFP, DPA, APE)