1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu zaidi ya 130 wenye virusi vya ukimwi waomba hifadhi nchini Canada

Gregoire Nijimbere4 Septemba 2006

Mkutano wa kimataifa juu ya ukimwi uliyofanyika mjini Toronto nchini Canada ulimalizika wiki uliopita lakini kuna taarifa kwamba watu 137 miongoni mwa waliyohudhuria mkutano huo, wameomba hifadhi nchini Canada. Watu hao ambao wengi wao ni kutoka nchini Afrika ya kusini, wametoa hoja kwamba wanabaguliwa nyumbani kwao kutokana na kukamatwa na virusi vya ukimwi.

Wajumbe kwenye ukumbi wa mikutanoToronto
Wajumbe kwenye ukumbi wa mikutanoToronto

Kulingana na taarifa kutoka Canada, kundi la watu 150 miongoni mwa wajumbe waliohudhuria mkutano huo wa kimataifa wa mjini Toronto, hawakutaka kurudi nyumbani. Badala yake wameomba hifadhi nchini Canada. Wanasema kuwa nyumbani kwao wanabaguliwa. Siku tatu zilizopita, wizara ya Canada inayohusika na maswala ya uhamiaji ilitangaza tu kuwa watu kiasi ya 40 waliomba ukimbizi.

Wengi wa wajumbe hao wanaotafuta kubaki nchini Canada ni kutoka nchini Afrika ya kusini. Kuna pia idadi dogo kutoka Eritrea, Salvador na Uganda.

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya Afrika ya kusini Ronnie Mamoep, amesema kuwa wamepata taarifa kwamba kundi la watu 150 wameomba hifadhi nchini Canada ila bado wanazichunguza taarifa hizo. Na kwamba wajumbe wa serikali waliyoko huko Canada, wameiomba serikali ya Canada kuzichunguza faili za watu hao na nchi wanakotokea, ila kwamba wanasubiri jibu kutoka kwa serikali ya Canada.

Hayo yametokea wakati ambapo nchini Afrika ya kusini kumezuka mjadala juu ya msimamo wa serikali wa kupuuza matumizi ya madawa ya kukabiliana na madhara ya virusi vya ukimwi. Serikali ya Afrika ya kusini imezidi kulaumiwa kwa msimamo wake wa sintofahamu dhidi ya ugonjwa wa ukimwi kama wanavyilalamika madaktari katika nchi hiyo yenye kuwa na idadi kubwa ya watu wanaokabiliwa na virusi vya ukimwi kuliko nchi yoyote yile.

Aidha madaktari wamemkosoa vikali waziri wa afya Manto Tshabalala- Msimang kuhusu kile wamekitaja ´´matamshi yasiyoeleweka ´´ na ´´mashauri ya kuleta hali ya sintofahamu´´ ambapo waziri huyo alisikika akitilia kipau mbele rishe tu na kupuuza umuhimu wa madawa katika juhudi za kupambana na ugonjwa wa ukimwi.

Mwenyekiti wa chama cha waganga nchini Afrika ya kusini daktari Kgosi Letlape, ameyajibu vikali matamshi ya waziri wa afya kwa kusema kwamba hadi sasa hamna suluhu jingine lililothibitishwa kisayansi dhidi ya virusi vya ukimwi mbali na kutumia madawa yale.

Alionya watu wasirudi kudanganywa.

Siku 10 zilizopita, mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa barani Afrika anayehusika na maswala ya ukimwi Stephen Lewis, aliilaumu pia serikali ya rais Thabo Mbeki kwamba inapuuza utoaji kwa raia madawa ya kupunguza madhara ya ukimwi. Aliyasema hayo katika sherehe za kuufunga mkutano wa kimataifa wa Toronto juu ya ukimwi.

Kulingana na baraza la utafiti wa kisayansi nchini Afrika ya kusini, watu laki tatu na alfu 26 walikufa kutokana na madhara ya ukimwi katika muda wa mwaka mmoja tu uliopita.

Kama alivyoelezea mbele ya bunge mwenyekiti wa baraza hilo Tony Mbewu, hata madaktari huwa wanasita mara fulani kuandika kwamba mtu amekufa kwa ukimwi. Hali hiyo amemalizia kusema, inasababisha hata kutoweza kujua takwim halisi kuhusiana na hali ya ukimwi nchini humo Afrika ya kusini.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW