1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu zaidi ya 180,00 wakimbia mapigano mapya Sudan Kusini

Zainab Aziz Chanzo: AFP
25 Januari 2026

Shirika la kibinadamu la Umoja wa Mataifa OCHA limesema, zaidi ya watu 180,000 wameyakimbia makazi yao katika kaunti nne za jimbo la Jonglei,la kaskazini mwa Juba,mji mkuu wa Sudan kusini kutokana na mapigano mapya.

Sudan kusini| Raia wa Sudan Kusini wanaokimbia mapigano mapya
Raia wa Sudan Kusini wanaokimbia mapigano mapyaPicha: LUIS TATO/AFP

Shirika la kibinadamu la Umoja wa Mataifa OCHA limesema haiwezekani kukadiria idadi ya watu waliokufa kwenye mapigano hayo kwa sababu wenyeji wengi bado wamejificha porini. 

OCHA imesema watu wengi wanaishi chini ya miti huku mali kwenye nyumba zao na hata kwenye vituo vya afya zimeporwa au kuchomwa moto na sasa watu hao wanakabiliwa na njaa kubwa. Maafa hayo yanaripotiwa kufanywa na pande zote mbili, hatua ambayo imelazimisha shirika hilo kusimamisha huduma muhimu za afya kwa maelfu ya watu.

Mapigano makali yalitokea wiki iliyopita katika eneo hilo wakati vikosi vya upinzani vilipochukua udhibiti, ingawa baadae vilifurushwa na wanajeshi wa serikali. 

Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir MayarditPicha: Abubaker Lubowa/REUTERS

Barney Afako, mjumbe wa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, katika taarifa yake amesema kinachoshuhudiwa Jonglei ni ongezeko la hatari ya usalama katika eneo hilo na sehemu nyingine za nchi. 

Ameonya kuwa vitendo vinavyotokea katika mkoa wa Jonglei vinaweza kuitumbukiza Sudan Kusini katika mzunguko mwingine hatari wa vurugu wakati amani dhaifu iliyo kuwepo ikiendelea kufifia.

Mashuhuda wameelezea matumizi yasiyo ya lazima ya mabomu hali iliyowalazimu baadhi ya raia kukimbilia kwenye madimbwi yenye maji mengi ili kujinusuru.

Nchi hiyo changa zaidi duniani inakumbwa na vita, umaskini na ufisadi mkubwa tangu ilipoanzishwa mnamo mwaka 2011 na vurugu zinaongezeka kati ya makundi hasimu, ambazo kwa sasa zimeingia kwenye jimbo la Jonglei.

Makubaliano ya kugawana madaraka kati ya pande mbili kuu yamekufa kabisa baada ya Rais Salva Kiir kumgeuka makamu wake wa rais na mpinzani wake wa muda mrefu, Riek Machar, ambaye alikamatwa mwezi Machi mwaka uliopita na sasa anakabiliwa na mashtaka ya "uhalifu dhidi ya ubinadamu".

Vikosi vya pande hizo mbili vimepigana mara kadhaa katika mwaka uliopita, lakini mapigano makubwa zaidi yalianza mwishoni mwa Desemba huko Jonglei.

Kiir na Machar waliingia vitani kwa miaka mitano muda mfupi baada ya uhuru wa Sudan Kusini vita ambavyo vilisababisha vifo vya watu 400,000. Mkataba wa kugawana madaraka wa mwaka 2018 ulidumisha amani kwa miaka kadhaa, lakini mipango ya kufanya uchaguzi na kuunganisha majeshi yao haikutimia.

Makamu wa Rais wa Sudan Kusini Riek Machar Picha: Samir Bol/REUTERS

Sudan Kusini ina akiba kubwa ya mafuta, lakini ufisadi mkubwa umeiacha nchi hiyo kuwa miongoni mwa mataifa maskini zaidi duniani. Kulingana na takwimu za Shirika la Mpango wa Chakula Duniani za mwezi Aprili mwaka uliopita karibu raia milioni 7.7 kati ya raia wanaokadiriwa kuwa milioni 12 wanakabiliwa na njaa kubwa. 

Chanzo kingine cha mashirika yasiyo ya kiserikali kimesema mabomu yalipiga  mita 100 hadi 200 katika maeneo yenye vituo vya afya.

Kongozi wa asasi za kiraia, Bol Deng Bol, amesema sehemu kubwa ya jimbo la Jonglei imewekwa kuwa ni eneo hatari na hii imaanisha kwamba ni eneo ambalo huduma za kibinadamu haziwezi kufikishwa na wala hakuna safari za ndege.

 

     

    

    

   

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW