Somalia
11 Februari 2010Watu wasiopungua 30 wameuawa mjini Mogadishu kutokana na mapambano baina ya majeshi ya serikali na wapinzani wa kiislamu.
Maafisa wa serikali pia wamearifu kwamba watu wengine zaidi ya 60 wamejeruhiwa katika mapambano hayo yaliyopamba moto tokea jana.
Wanajeshi wa serikali ya Somalia walitumia mizinga kuzishambulia sehemu za wapinzani katika soko la Bakara- sehemu ambapo watu wengi wanaishi.
Majeshi ya serikali yalichukua hatua baada ya kushambuliwa na wapinzani hapo jana.
Habari zinasema watu wasiopungua 30 wameuawa tokea jana na wengine zaidi ya 60 wamejeruhiwa katika mapigano hayo.
Daktari mmoja kwenye hospitali ya Madina mjini Mogadishu amesema hospitali yao imepokea majeruhi 61. Daktari huyo aliliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kuwa watu watatu walikufa muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini.Watu hao walikufa wakati walipokuwa wanatibiwa.
Kundi la wapinzani al-Shabaab ambalo hivi karibuni lilitangaza kujiunga na mtanda wa al-qaida limepania kuing'oa serikali dhaifu ya Somalia inayoungwa mkono na nchi za magharibi. Wapinzani hao wanaidhibiti sehemu kubwa ya mji mkuu- Mogadishu pamoja na sehemu za kusini na za kati nchini Somalia.
Radio Shabelle imeripoti kwamba sehemu kadha za mji wa Mogadishu zimeshambuliwa kwa makombora, na mamia ya raia wanayakimbia mapigano hayo baina ya majeshi ya serikali na wapinzani wa al-Shabaab. Msemaji wa kitengo cha misaada amelalamika kwamba majeshi ya serikali na wapiganaji wa al-Shabaab wameweka vizuizi vinavyozuia kutolewa kwa huduma za haraka kwa majeruhi ambao wangeliweza kupelekwa haraka kwenye hospitali ambazo bado zinafanya kazi mjini Mogadishu.
Msemaji huyo amezitaka pande zinazopigana ziyaruhusu magari ya kuwahudumia wagonjwa yapite.
Katika siku za hivi karibuni mamia ya wapiganaji wa al-Shabaab wamekuwa wanamiminikia katika mji wa Mogadishu.
Serikali ya mpito nchini Somalia inayoongozwa na rais Sheikh Sharif Sheikh Ahmed mwenye mtazamo wa ukadirifu inategemea msaada wa wanajeshi wapatao 5200 wa Umoja wa Afrika.
Hatahivyo wanajeshi hao wanalinda usalama wa sehemu ya makao ya serikali na usalama wa uwanja wa ndege.
Mwandishi /Mtullya Abdu/ZA /DPA.
Mhariri/Abdul-Rahman