1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watu zaidi ya 30 wauwawa katika shambulizi la Urusi, Ukraine

8 Julai 2024

Mashambulizi makubwa ya makombora ya Urusi katika miji kadhaa ya Ukraine yamewaua watu 31 na kuwajeruhi wengine zaidi ya 150, huku kombora moja likitua katika hospitali inayohudumia watoto katika mji mkuu wa Kiev.

Ukraine Kyjiw 2024 | Russischer Raketenangriff auf Kinderkrankenhaus Okhmatdyt
Picha: Efrem Lukatsky/AP Photo/picture alliance

Waokoaji wameendelea na juhudi za kutafuta manusura chini ya vifusi katika majengo ya hospitali hiyo ya watoto yaliyoharibiwa.

Mashambulizi hayo yameilenga miji mitano ya Ukraine huku makombora tofauti zaidi ya 40 yakiharibu majengo ya makaazi na miundombinu ya umma.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy amesema nchi yake italipiza kisasi kufuatia mashambulizi hayo ambayo yamesababisha vifo vya watu 31 huku wengine zaidi ya 150 wakijeruhiwa vibaya. 

Zelenskiy ambaye yuko ziarani mjini Warsaw ambako pia amesaini mkataba wa usalama na Poland ametoa pia wito wa kufanyika mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kufuatia mashambulizi hayo.

Hospitali ya watoto ya Okhmatdyt mjini Kiev pia imeshambuliwa kwa makombora kutoka Urusi. Zelensky amesema makombora 40 yalirushwa katika maeneo tofauti ya Ukraine.

Shambulizi hilo linafanyika wakati viongozi wa Jumuiya ya kujihami ya NATO wakijiandaa kukutana mjini Washington kwenye mkutano wao wa kilele wa kusherehekea miaka 75 ya muungano huo.

Zelenskiy amewatolea wito washirika wake wa Magharibi kutoa jibu thabiti kwa mashambulizi hayo ya Urusi.

Urusi yakisahambulia kwa droni kituo cha nishati cha Sumy

Wakati huo huo, waziri Mkuu wa India Narendra Modi amewasili mjini Moscow ili kuanza ziara ya siku mbili nchini Urusi ambapo anatazamiwa pia kufanya mazungumzo na rais Vladimir Putin na kujadiliana kuhusu vita vya Ukraine.

afp/ap