Watu zaidi ya 30 wauwawa mashariki mwa Kongo
8 Juni 2014Wahanga, wakiwemo wanawake wajawazito, walikuwa wamepigwa risasi, kudungwa visu au kuchomwa moto ndani ya nyumba zao. Mpigapicha wa shirika la habari la Reuters katika eneo la tukio katika kijiji cha Mutarule alihesabu maiti 37, baadhi zikiwa zimezagaa ndani ya kanisa la kijiji hicho, kinachopatikana kilometa takriban 50 kutoka Bukavu, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kusini.
Wakaazi na viongozi wa dini wamesema wagonjwa waliokuwa katika kituo cha matibabu walishambuliwa. Mbali na waliouwawa, watu wengine zaidi ya 20 walijeruhiwa, huku 10 kati yao wakiwa katika hali mahututi.
"Ni raia wa Kongo waliofanya mashambulizi haya. Yanahusiana na mzozo juu ya ngo'mbe," amesema gavana wa jimbo la Kivu Kusini, Mercellin Cishambo, wakati alipozungumza na shirika la habari la Reuters. "Tatizo ni kwamba kila mtu katika eneo hili hubeba silaha." Gavana huyo amekadiria idadi ya watu waliouwawa kuwa 27.
Msemaji wa serikali ya Kongo, Lambert Mende, amesema tukio hilo lilikuwa shambulizi la kulipiza kisasi lililofanywa na jamii ya mchunga ng'ombe mmoja aliyeuwawa wakati wa jaribio la kuiba ng'ombe waliomilikiwa na mkulima mwingine. "Kamanda wa jeshi katika eneo hilo ametiwa mbaroni kwa sababu alichukua hatua za taratibu mno. Anazuiliwa na polisi. Maafisa pia wamemkamata kiongozi mmoja wa eneo hilo anayeshukiwa kuratibu mashambulizi hayo," akaongeza kusema Mende. Mende aidha amesema idadi ya watu waliouwawa katika machafuko hayo ni 34.
Shambulizi la pili
Jimbo la Kivu Kusini, eneo la milima lenye utajiri wa madini ikiwemo dhahabu, ni makazi kwa jamii za makabila yaliyoikimbia nchi jirani ya Burundi baada ya kumalizika vita vya wenyewe kwa wenyewe mnamo mwaka 2005 na vile vile makundi mengi ya waasi, likiwemo kundi linalopigania ukombozi wa Rwanda, FDLR.
Baadhi ya wanakijiji kutoka kabila la Bafuliru nchini Kongo wamewalaumu waasi kutoka Burundi wa kundi la FNL kwa mashambulizi hayo. Wakaazi wamesema mwezi Agosti mwaka uliopita watu wanane waliuwawa na watu wasiojulikana waliokuwa wamejihami na silaha katika kijiji hicho. Kaburi lenye misalaba minane ndio ishara inayoonyesha mahala walipozikwa watu hao.
"Mauaji ya kwanza ya kiholela yalitokea, na sasa la pili limetokea na hatujafahamu kilichotokea wakati wa mauaji ya kwanza," mzee wa mtaa Amuri Kikukama ameliambia shirika la habari la Reuters. "Tunashangaa kwa nini mauaji yanapaswa kuendelea huku serikali ikitazama tu."
Mkaazi mwingine wa pili amesema kundi la waasi wenye silaha wana kambi yao yapata kilometa 20 kutoka kijiji hicho cha Mutarule. Wanakikiji wengi walikuwa wakifungasha virago vyao siku ya Jumamosi kuondoka kwenda katika kijiji kingine.
Tume ya MONUSCO yachukua hatua
Tume ya amani ya Umoja wa Mataifa nchini Kongo, MONUSCO, ilitoa taarifa Jumamosi jioni ikisema mapigano makali yalikuwa yametokea usiku wa kuamkia jana kati ya jamii ya Bafuliru kwa upande mmoja na jamii za Barundi na Banyamulenge kwa upande mwingine. Wabarundi na Wabanyamulenge ni Watutsi kutoka Burundi ambao wamekuwa wakiishi Kivu Kusini kwa vizazi kadhaa. Kumekuwa na mzozo kati ya Wabafuliru na Wabarundi kuhusiana na mali za masuala ya mila.
Martin Kobler, Mkuu wa tume ya MONUSCO, amesema tume hiyo inatuma wanajeshi zaidi kuwalinda raia. "Vitendo hivi vya umwagaji damu havikubaliki na lazima vikome mara moja," akasema Kobler katika taarifa yake. Wanajeshi wa kulinda amani wa tume hiyo wametumwa Mutarule kuwaondoa watu waliojeruhiwa na kuwasaidia maafisa wa eneo hilo na jeshi la Kongo kurejesha utulivu.
Serikali ya Kongo imesema inapanga kuwashambulia waasi kutoka nje ya nchi wanaoendesha shughuli zao mashariki mwa taifa hilo baada ya kushindwa kundi la waasi wa M23 mwishoni mwa mwaka jana.
Mwandishi: Josephat Charo/RTRE
Mhariri: Sekione Kitojo