1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watuhumiwa 25 wa ugaidi wakamatwa Ujerumani

7 Desemba 2022

Polisi nchini Ujerumani wamewatia nguvuni zaidi ya watu 20 wanaoshukiwa kuwa wafuasi wa kundi la siasa kali za mrengo wa kulia lenye azma ya kupinduwa serikali kwa njia ya silaha kufuatia msako uliofanyika nchi nzima.

Razzia gegen Reichsbürger-Szene - Frankfurt Main
Picha: Boris Roessler/picture alliance/dpa

Waendesha mashitaka wa serikali kuu ya shirikisho walisema maafisa 3,000 wa polisi walifanya msako siku ya Jumatano (Disemba 7) kwenye maeneo 130 ndani ya majimbo 11 kati ya 16 ya Ujerumani dhidi ya wafuasi wa kundi vuguvugu lijiitalo Reichsbürger, ambalo linapingana na katiba ya sasa ya Ujerumani na linalotaka kuiangusha serikali.

Waziri wa Sheria, Marco Buschmann, aliuita uvamizi huo kuwa ni "operesheni dhidi ya ugaidi", akiongeza kwamba inawezekana watuhumiwa hao walikuwa wamepanga mashambulizi dhidi ya taasisi za serikali wakitumia silaha.

Waendesha mashitaka walisema raia 22 wa Kijerumani walitiwa nguvuni kwa kushukiwa kuwa wanachama wa kundi hilo la kigaidi, huku wengine watatu - mmoja wao akiwa raia wa Urusi - wakishukiwa kulisaidia kundi hilo.

Wanajeshi wahusika

Maafisa wa polisi ya Ujerumani kwenye msako dhidi ya wanachama wa kundi la Reichsbürger mjini Frankfurt siku ya tarehe 7 Disemba 2022.Picha: Boris Roessler/picture alliance/dpa

Gazeti la kila wiki la Der Spiegel liliripoti kwamba maeneo yaliyofanyiwa msako ni pamoja na kambi za kijeshi za kikosi maalum cha KSK katika mji wa kusini magharibi wa Calw.

Kikosi hicho kimekuwa kikishutumiwa kuwa baadhi ya wanajeshi wake wanajihusisha na siasa kali za mrengo wa kulia.

Hata hivyo, waendesha mashitaka wa serikali kuu walikataa kuthibitisha ama kukanusha kwamba kambi hizo za wanajeshi zilihusishwa kwenye msako huo.

Mbali na waliowekwa kizuizini nchini Ujerumani, waendesha mashitaka wanasema mtu mmoja alikamatwa katika mji wa Kitzbuehel ulioko nchini Austria na mwengine katika mji wa Preguia ulioko Italia.

Tuhuma dhidi ya kundi la Reichsbürger

Waendesha mashitaka hao walisema waliokamatwa wanatuhumiwa "kuunda kundi la kigaidi mwaka jana kwa lengo la kuuondoa mfumo wa serikali ya sasa ya Ujerumani na kuweka wao wenyewe, huku wakijuwa kuwa lengo lao linaweza tu kutimizwa kwa kutumia njia za kijeshi na silaha."

Mmoja wa wafuasi wakubwa wa kundi la Reichsbürger, Joachim Widera, akishikilia anayosema ni paspoti ya dola 'jipya' la Ujerumani.Picha: Picture-Alliance/dpa/P. Seeger

Watu hao wanasemekana wanaamini kwenye nadharia za upotoshaji juu ya simulizi za kile kiitwacho Raia wa Himaya ya Kifalme na pia itikadi ya QAnon.

Waendesha mashitaka walisema kuwa wanachama wa kundi hilo wanaamini kuwa Ujerumani inatawaliwa na kile kiitwacho "deep state" - ama dola la siri, madai kama yale yanayotolewa na rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump.

Waendesha mashitaka waliwataja viongozi wa kundi hilo kuwa ni Heinrich XIII P.R na Ruediger v. P. Gazeti la Der Spiegel liliripoti kwamba Heinrich ni mzee wa miaka 71 kutoka familia ya watu mashuhuri, huku mwenzake akiwa mwanajeshi mstaafu mwenye umri wa miaka 69.

Kwa mujibu wa waendesha mashitaka, Heinrich, ambaye kundi hilo lilipanga kumuweka kama kiongozi mpya wa Ujerumani, aliwahi kufanya mawasiliano na maafisa wa Urusi kwa lengo la kufikia makubaliano juu ya mfumo mpya wa nchi mara tu serikali ya Ujerumani ikishapinduliwa.