Watuhumiwa wa uhalifu katika jimbo la Darfur watajwa mjini The Hague.
27 Februari 2007Mtuhumiwa huyo Ahmed Harun ambae sasa ni waziri wa masuala ya kibinadamu,alikuwa waziri wa mambo ya ndani alieshughulikia mgogoro wa Darfur.Anakabiliwa na tuhuma za kusaidia katika kuandikisha wanamgambo waliofanya mauaji, waliobaka na kutesa raia.
Mtuhumiwa mwengine Ali Abdalrahman aliekuwa kiongozi wa wanamgambo wa Janjaweed anakabiliwa na tuhuma za kufanya mashambulio katika vijiji vitatu vya jimbo la Darfur.
Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama kuu ya mjini The Hague Luis Moreno Ocampo amewataka mahakimu watoe waranti ili watuhumiwa hao walifikishwe mahakamani. Mwendesha mashtaka huyo amesema kuwa watu hao wanahusika na uhalifu dhidi ya binadamu pamoja na uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur mnamo miaka ya 2003 na 2004.
Mapema mwezi machi mnamo mwaka 2005 Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliiomba mahakama hiyo ya kimataifa ifanye uchunguzi juu ya uhalifu unaofanyika katika sehemu hiyo. Lakini serikali ya Sudan wakati wowote imekuwa inapinga kufanyika uchunguzi wowote.
Watu wapatao laki mbili wameshauawa katika jimbo la Darfur na wengine zaidi ya milioni mbili wamelazimika kuyahama makao yao tokea mwaka 2003 ambapo mgogoro wa Darfur ulifumuka . .Waasi wa jimbo hilo wanapambana na serikali ya Sudan tokea wakati huo.
Ripoti kadhaa za kimataifa pamoja na wataalamu wameambatanisha ukatili unaofanyika katika jimbo hilo na kampeni ya wanamgambo wa Janjaweed wanaoungwa mkono na serikali ya Sudan.
Wanamgambo hao wamefanya mashambulio katika vijiji kadhaa vya raia.
Lakini rais Omar al Bashir wa Sudan anakanusha kuhusika kwa serikaki yake katika ukatili unaofanyika katika jimbo la Darfur na amesema kuwa taarifa juu ya mgororo huo wa jimbo hilo zimetiwa chumvi na Marekani.
Na kwa mujibu wa gazeti moja la nchini Sudan Akbar el Yum ,serikali ya Sudan imesema kuwa haitaitambua mahakama hiyo ya kimataifa ya mjini the Hague.
Lakini msemaji wa kitengo cha misaada ya maendeleoa cha Umoja wa Ulaya Amedu Altafaj amesema kuwa kila uhalifu lazima uadhibiwe.
Lazima tuwasilishe ujumbe, sisi kama jumuiya ya kimataifa , kwamba hakuna uhalifu utakaofanyika bila ya kuadhibiwa.Hayo ni lazima , siyo tu kwa Darfur bali pia kuhusu migogoro yote duniani , na hasa barani Afrika.Hapana budi ifahamike kwamba ,yeyote anaekiuka haki za binadamu lazima atahukumiwa.
Mwendesha mashtaka mkuu wa mahakama ya kimataifa ya mjini the Hague Luis Moreno Ocampo ametumia muda wa miaka miwili kuchunguza ushahidi uliokusanywa na jopo la Umoja wa Mataifa baada ya Baraza la Usalama kupitisha hoja ya kuwasilisha kwake majina 51 ya watuhumiwa.
Bwana Ocampo ameeleza kuwa uhalifu uliotendwa ni pamoja na mauaji,mateso,matendo ya ubakaji na uharamia . Jopo la Umoja wa Mataifa pia limewasilisha ushahidi juu ya raia walilazimika kuyahama makao yao.
Bwana Moreno Ocampo amesema anatumai kwamba kazi ya mahakama yake itasaidia kuzuia uhalifu katika siku za usoni.
Na ABDU MTULLYA.