1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Watuhumiwa wakamatwa Ugiriki wakati msako ukiendelea Ulaya

18 Januari 2015

Wakati Ulaya iko ukingoni, wanajeshi wakiwekwa kulinda maeneo ambayo magaidi wanaweza kushambulia nchini Ubelgiji,polisi nchini Ugiriki wamewakamata kiasi washukiwa wawili.

Belgien Antwerpen Sicherheit Terrorismus
Wanajeshi wakilinda mitaa nchini UbelgijiPicha: picture-alliance/dpa/Nicolas Maeterlinck

Hii ni sehemu ya mapambano yanayoendelea dhidi ya ugaidi katika bara Ulaya.

Nchini Ufaransa , mmoja kati ya magaidi waliohusika katika mashambulio ya wiki iliyopita mjini Paris amezikwa kwa siri wakati maafisa wakijaribu kuzuwia kuutukuza ugaidi na ghasia kwa umma huku kukiongezeka upinzani katika bara la Ulaya dhidi ya Uislamu, na maandamano dhidi ya dhihaka kwa Mtume Muhammad katika mataifa ya Kiislamu yakionesha tofauti kubwa miongoni mwa tamaduni.

Wanajeshi na polisi wakilinda doria UbelgijiPicha: picture-alliance/dpa/Nicolas Maeterlinck

Kwa mara ya kwanza katika miongo mitatu, maafisa wametumia wanajeshi kuimarisha jeshi la polisi katika miji nchini Ubelgiji, wakilinda majengo katika maeneo ya Wayahudi katika mji wa bandari wa Antwerp na baadhi ya balozi nchini humo. Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya msako wa kupambana na ugaidi kuwanasa washukiwa kadhaa katika Ulaya magharibi na kuongeza hisia za wasi wasi katika maeneo mengi ya eneo hilo.

Tahadhari yaongezwa

Ubelgiji imeongeza tahadhari yake ya ugaidi kufikia kiwango cha tatu, ikiwa ni nafasi ya juu ya pili kufuatia misako ya kupambana na ugaidi siku ya Alhamis ambapo washukiwa wawili wameuwawa. Polisi wanaamini kundi ambalo kwa kiasi kikubwa wamelivunja lilikuwa karibu ya kufanya mashambulizi makubwa.

Maafisa wamesema kwamba licha ya kulivunja kundi hilo bado wanawatafuta washukiwa wengine nje ya nchi hiyo na kwa muda wanamatumaini kuwa Ugiriki inaweza kuwa imewakamata watu wengine muhimu ambao wanatafutwa.

Maandamano ya kuwakumbuka waliouwawa mjini ParisPicha: picture-alliance/dpa/Jensen

Afisa wa polisi ya Ugiriki mapema jana Jumamosi amesema watu hao walikamatwa tofauti mjini Athens, kiasi ya kilometa 2,500 kutoka mjini Brussels, na wanajumuisha mtu mmoja ambaye kwa kumwangalia anafanana na maelezo yanayotolewa kwa mtuhumiwa muhimu wa ugaidi nchini Ubelgiji.

Afisa huyo amezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina kutokana na unyeti wa uchunguzi unaoendelea.

Baada ya uchunguzi wa kina wa taarifa za utambulisho , mwendesha mashtaka mkuu wa Ubelgiji Eric Van der Sypt amesema hakuna uhusiano unaotambulika na mtu huyo ambaye anatafutwa na kusema "hana uhusiano na suala la Ubelgiji."

Ubelgiji imeweka wanajeshi wa kwanza 150 kulinda maeneo kadhaa nchini humo.

Wakati baadhi ya washukiwa wakiwa hawajulikani waliko , kuna hali ya utulivu yenye wasi wasi nchini Ubelgiji , na wanajeshi katika mitaa sio lazima kuwa wanasaidia.

"Unafahamu, wakati watu wanawaona wanajeshi mitaani wanapata hofu. Hii inaweza kusababisha matatizo zaidi kuliko suluhisho," amesema mwanafunzi Greg Verhoeven mjini Antwerp.

Maandamano ya kupinga vibonzo vinavyomdhihaki Mtume Muhammad nchini JordanPicha: Reuters/M. Hamed

Washambuliaji wazikwa

Ufaransa imejaribu kuondoa hali ya ghasia wakati Said Kouachi , mmoja kati ya watu waliokuwa na silaha ambao walishambulia ofisi za jarida la vikatuni vya dhihaka la Charlie Hebdo , walizikwa kimya kimya.

Baada ya awali kukataliwa kutolewa nafasi ya kuzikwa Kouachi , meya wa mji wa Reims, Arnaud Robinet , amesema amelazimika kubadilisha msimamo wake.

Robinet amesema serikali imesisitiza aruhusu kaka mkubwa azikwe Reims kwasababu kwa mujibu wa sheria za Ufaransa wakaazi wa mji wana haki ya kuzikwa hapo.

"Alizikwa jana usiku, katika usiri mkubwa na mahali ambapo hapatambuliki kwa kadri inavyowezekana," Robinet amesema.

Wakati huo huo watu watano wameuwawa na makanisa kuchomwa moto nchini Niger jana Jumamosi(17.01.2015) katika maandamano mapya dhidi ya jarida la kila wiki nchini Ufaransa la Charlie Hebdo lililochapisha toleo lake lenye katuni inayomwonesha mtume Muhammad katika ukurasa wake wa mbele, wakati Ufaransa ikishutumu ghasia hizo na kutetea uhuru wa kujieleza.

Waandamanaji wanapinga vobonzo vinavyomdhihaki Mtume Múhammad nchini AlgeriaPicha: picture-alliance/dpa

Idadi ya watu waliokufa katika ghasia siku moja iliyopita katika mji wa pili nchini Niger wa Zinder imepanda kutoka wanne hadi watano baada ya mwili wa mtu kupatikana "ukiwa umechomwa moto katika kanisa", amesema rais wa Niger Mahamadou Issoufou katika hotuba yake kwa taifa, wakati akitoa wito wa utulivu.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Ufaransa laurent Fabius ameshutumu "matumizi ya nguvu" nchini Niger wakati rais Francois Hollande amesema Ufaransa inajikita katika kutetea "uhuru wa kujieleza", na kusema hilo halina mjadala".

Kiasi ya watu 15,000 wameandamana katika eneo la kaukasus kaskazini la Urusi nchini Ingushetia dhidi ya vibonzo vya Charlie Hebdo , ambalo limemchora mtume Muhammad akilia huku ameshikilia karatasi iliyoandikwa maneno "Mimi ni Charlie".

Pia kumekuwa na maandamano nchini Pakistan siku ya Ijumaa, na katika ukanda wa Gaza kituo cha utamaduni cha Ufaransa kimechafuliwa kwa michoro ya graffiti , inayosema : "Mtakwenda motoni , waandishi wa Ufaransa".

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / ape

Mhariri: Abdu Mtullya