1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UgaidiAfrika

Watuhumiwa wawili wa Westgate wakutwa na hatia, moja aachiwa

Thelma Mwadzaya7 Oktoba 2020

Mahakama mjini Nairobi imewatia hatiani Mohamed Ahmed na Hussein Hassan Mustafa kwa makosa ya kula njama ya kutenda kitendo cha ugaidi na kuwa na vitu vinavyoendeleza shughuli za ugaidi. Mshukiwa wa tatu ameachiwa huru.

Hussein Hassan Mustafah, Liban Abdullah Omar, Mohamed Ahmed Abdi
Picha: Brian Inganga/AP Photo/picture-alliance

Mahakama imewatia hatiani watuhumiwa wawili wa shambulio la kigaidi katika jengo la  maduka la Westgate lililotokea miaka 7 iliyopita jijini Nairobi. Mtuhumiwa wa tatu ameachiliwa huru kwa ukosefu wa ushahidi kamili.

Shambulio la kigaidi la Westgate liliwaua watu 67 na wengine zaidi ya 100 walijeruhiwa mwaka 2013.

Watuhumiwa wawili Mohamed Ahmed na Hussein Hassan Mustafa wamepatikana na hatia kwa kuhusika na kufanikisha ugaidi kwa kudhamiria, huku mtuhumiwa wa tatu Liban Omar akiachiliwa huru kwa kukosa ushaidi kamili.

Washtakiwa wa shambulio la Westgate wakiwasili mahakamani mjini Nairobi, Oktoba 5, 2020.Picha: Brian Inganga/AP Photo/picture-alliance

Mahakama imeamuru mtuhumiwa huyo ambaye ni mkimbizi apewe kadi yake maalum na kumkabidhi kwa maafisa wa shirika la Umoja wa Mataifa la Wakimbizi,UNHCR.

Soma pia: Nairobi: Westgate Mall lafunguliwa upya

Watatu hao walifika mbele ya hakimu mkuu Francis Andayi kwenye mahakama ya Milimani kujibu mashtaka 12 ya kuhusika na kitendo cha ugaidi, kumiliki mali ya wizi na kuwa ndani ya mipaka ya Kenya kinyume na sheria.

Kulikuwa na ulinzi mkali kwenye mahakama ya Milimani jijini Nairobi wakati kesi ya uhalifu uliosababisha shambulizi la kigaidi kutokea miaka 7 iliyopita kwenye jengo la biashara la Westgate mtaani Westlands.

Wanajeshi wakijipanga kuingia jengo la Westgate wakati wa shambulio la Septemba 24, 2013, ambamo watu 67 walipoteza maisha.Picha: picture-alliance/AP Photo

Watatu hao walishtakiwa mmoja mmoja kwa mara ya kwanza mwezi Novemba mwaka 2013. Mshukiwa wa nne Adan Dheq aliachiliwa huru mwezi Januari mwaka 2019 baada ya upande wa mashtaka kushindwa kumbana kwa kukosa ushahidi kamili. Zaidi ya mashahidi 145 walifika mbele ya mahakama kujieleza.

Soma pia: Kenya yalaumiwa kutojibu haraka mashambulizi

Upande wa mashtaka waomba hukukumu icheleweshwe

Wakati huohuo upande wa mashtaka umeiomba mahakama kusubiri kabla kutangaza hukumu ili kuwapa nafasi waathiriwa wa shambulio la Westgate kuandika taarifa zao. Mwaka 2015 ripoti ya polisi ilibaini kuwa kundi la kigaidi la Al Shabaab lilipanga na kutekeleza shambulio hilo.

Duru rasmi za idara ya ujasusi ya Kenya, NIS, ziliashiria kuwa Gaarar ambaye ni raia wa Somalia ndiye aliyenunua gari dogo aina ya Mitsubishi lenye nambari ya usajili ya KAS 575X lililokamatwa mbele ya jengo la Westgate baada ya shambulio. Gari hilo lilikuwa limesheheni silaha na zana za kulipuka na kupatikana wiki moja baada ya tukio.

Moshi ukifuka juu ya jengo la maduka la Westgate, kufuatia shambulio la kigaidi la Septemba 23, 2013. Mahakama imewatia hatiani washukiwa wawili wa shambulio hilo.Picha: Reuters

Kulingana na Inspekta mkuu wa polisi wa wakati huo Joseph Boinnet, Garaar na wenzake waliuawa tarehe 12 mwezi wa Machi pale Marekani iliposhambulia Somalia kwa ndege zisizokuwa na rubani.

Soma pia: Kenya yatangaza majina ya magaidi

Shambulio jengine lilitokea kwenye chuo kikuu cha Garissa pale watu 148 wengi wao wanafunzi walipouawa kinyama mwanzoni mwa Aprili mwaka 2015. Hukumu dhidi ya washtakiwa imepangiwa tarehe 22 mwezi huu wa Oktoba.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW