1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waumini milioni moja washiriki misa ya Papa, Kongo

1 Februari 2023

Zaidi ya waumini milioni moja huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameshiriki ibada iliyoongozwa na kiongozi wa kanisa hilo Papa Francis katika mji mkuu Kinshasa.

DR Kongo Papstmesse in Kinshasa
Picha: Arsene Mpiana/AFP

Waratibu wa misa hiyo ya Papa Francis wamesema zaidi ya waumini milioni moja walikuwepo kwenye uwanja wa ndege wa Ndolo ambako ibada hiyo imefanyika. Wengi wa waumini walianza kumiminika uwanjani hapo usiku wa jana, ili tu kujihakikishia kwamba wanapata nafasi ya kukaa. Adrien Louka, 55 aliliambia shirika la habari la AFP kwamba aliwasili kwenye viwanja hivyo tangu saa 11 za alfajiri.

Papa Francis aliwasili kwenye viwanja hivyo akiwa kwenye gari maalumu na kulakiwa kwa nyimbo na makundi ya watu waliokuwa wakicheza ngoma za aina mbalimbali kabla ya kuanza kwa ibada hiyo majira ya saa 3.30 asubuhi.

Soma Zaidi:Papa Francis awasili Kongo, akianza ziara ya siku sita 

Wakazi wa eneo hilo wameliambia shirika la AFP kwamba wanaichukulia ziara hiyo kama hatua muhimu ya maridhiano katika taifa hilo linalokabiliwa na machafuko na hasa kupitia ujumbe utakaotolewa na Papa kwenye misa hiyo na kuliacha taifa hilo likiwa na amani.

Rais Felix Tshisekedi pia alihudhuria misa hiyo pamoja na viongozi wakuu wa upinzani.

Sehemu ya waumini walioshiriki ibada ya misa iliyoongozwa na Papa Francis huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Guerchom Ndebo/AFP

Papa Francis kwenye ibada hiyo aliwatakia amani waumini akitumia lugha ya Lingala, ambayo ni moja kati ya lugha nne zinazotumiwa kila siku na wakazi wa Kinshasa. Kwa kiasi kikubwa ujumbe wake ulibeba dhima ya amani na kuwahimiza watu kuepuka migawanyiko.

Pamoja na waumini waliofika uwanjani hapo, wengi wa wakazi walijipanga mitaani kumsalimia Papa wakati anapopita.

Soma Zaidi: Papa Francis ayataka mataifa ya kigeni kuacha kuipora Kongo

Taifa hilo linakaliwa na karibu asilimia 40 hadi 49 ya waumini wa Kikristu, miongoni mwa karibu watu milioni 100. Asilimia 35 ni Waprotestanti na madhehebu mengine.

Papa Francis anatarajiwa pia kukutana na wahanga mzozo mashariki mwa Kongo na kisha kuzungumza na wawakilishi wa mashirika ya misaada.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inakabiliwa na idadi kubwa ya makundi yenye silaha na tangu mwishoni mwa mwaka 2021, kundi la wanamgabo la M23 pia limeyakamata maeneo makubwa ya jimbo la Kivu Kaskazini huku wakiusogelea mji wa Goma.

Kabla ya kufika Kongo, Papa Francis aliwaambia waandishi wa habari kwamba anatakamani sana kwenda kwenye mji huo wa Goma, lakini anatatizika kutokana na vita. Alisema "kwa kuwa kuna vita huwezi kwenda kule"

Siku ya Ijumaa Papa Francis atakwenda Juba, nchini Sudan Kusini.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW