Waumini wa Kiislamu Uganda walaani vita nchini Iran
20 Machi 2026
Kwenye msikiti wa Mawanga mtaa wa Munyonyo ambapo waumini wa Kiislamu kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Nigeria, Sudan na mataifa ya Mashariki ya Kati walipo hapa Uganda wameshiriki ibada maalum ya Idd ul Fitr kukamilisha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Katika hotuba yake, imam wa msikiti huo, Msomi Kasozi, ameongoza katika kulaani vita vya vya Mashariki ya Kati hasa vile kati ya muungano wa Marekani na Israel dhidi ya Iran, "Tunaposherehekea Idd ul Fitr tuwakumbuke ndugu zetu katika vita hivyo vya Marekani na Israel ambavyo tunavilaani vikali."
Hotuba za kulaani vita hivyo ndizo zilizotawala katika misikiti mbalimbali siku ya leo. Baadhi ya viongozi wa kidini na waumini wamevitaja kuwa vinatumiwa na mataifa kujaribisha zana zao za vita bila kujali madhara yake kwa ulimwengu.
Wamelezea kuwa vitahivyo ambavyo vilianza katika mwezi wa Ramadhan vimesababisha vifo vya watu wengi, kuwaacha wengi katika maisha ya mashaka na pia kusababisha uharibifu mkubwa wa makaazi na miundombinu.
Mkuu wa Utafiti katika chuo Kikuu cha Kampala International University Profesa Ibrahim Sani Madugu kutoka Nigeria ameimbia DW, "Katika karne hii ya 21, tuna vita kama hivi ambapo watu wasio na hatua wanauawa, ina maana tunaongea tu, lakini vitendo vyetu havionyeshi kama tumestaarabika.."
Viongozi wa Kiislamu na na baadhi ya waumini wamehimiza jamii ya kimataifa wasipotoshwe kuwa hivi vita ni dhidi ya Uislamu bali ni vita ambavyo havina msingi wowote na vimesababisha madhara makubwa kwa amani, usalama na uchumi wa dunia.
Ama baada ya Swala la Idd, waumini ambao wengi waliandamana kama familia kwenda kwenye misikiti na sehemu zingine zilizotengwa kwa ajili la ibada hiyo wameonekana wenye furaha na bashasha za Idd.