Wavulana 12 waliokwama pangoni Thailand wagundulika wako hai
3 Julai 2018Wavulana 12 na kocha wao wa mpira wa miguu wamegundulika wakiwa katika hali ya kukonda na wenye njaa kwenye lindi la tope lililozingirwa na maji usiku wa jana Jumatatu, na kuhitimisha zoezi la kuwasaka wachezaji hao chipukizi ambalo lilivuta hisia za watu. Lakini mwelekeo wa haraka hivi sasa umehamia katika kazi ngumu ya jinsi ya kuwaokoa salama kutoka kwenye pango hilo lililojaa maji.
Vyakula na vifaa vya matibabu vilihitajika sana na vilifanikiwa kuwafikia hii leo wakati waokoaji wakijiandaa kwa operesheni ndefu ya kuwaondoa. Jeshi la Thailand, limesema kwamba linatoa chakula cha kukidhi mwezi na somo la kupiga mbizi kwa wavulana hao ili kuwasaidia kuweza kutoka katika pango hilo la Tham Luang kaskazini mwa nchi.
Narongsak Osottanakorn ni gavana wa jimbo la Chiang Rai amesema kwamba, "tumetuma vyakula na virutubisho vingine vya nguvu. Kama dawa tumepeleka maji yenye chumvi, madawa ya kupambana na wadudu. Pia kulikuwa na dawa za kutuliza maumivu kama Paracetamol. Tumepeleka madawa ya msingi kama walivyopendekeza madkatari ya kuzuia wasipate maambukizi au maumivu. Tutakapowatoa pangoni tutawatizama hali zao ili wapelekwe hospitali. Tunatarajia kuwapeleka hospitali ya serikali ya jimbo la Chiang Rai."
Wavulana hao waligundulika jana Jumatatu saa nne usiku na wapiga mbizi wa Uingereza karibu mita 400 kutoka sehemu ambayo waliaminika kuwa wamekwama ikiwa ni kilometa kadhaa ndani ya pango hilo. Katika mkanda wa vidio uliorushwa kupitia ukurasa wa Facebook wa jeshi la majini la Thailand, mmoja wa wavulana hao alionekana akiwaomba waokoaji "kwenda nje."
Waokoaji hao wa Uingereza walimjibu "hapana, hapana, sio leo watu wengi wanakuja sisi ni wa kwanza" wakimaanisha operesheni kubwa na ngumu ya uokoaji inayofanywa juu ya vilima. Kazi ya kuwaokoa wavulana hao inakuwa ngumu kwa sababu vijana hao wapo katika hali mbaya na hawana uzoefu wa kupiga mbizi.
Njia ya umbali wa kilomita moja iliyojaa maji kuelekea lango la kuingilia itawachukua saa sita wapiga mbizi wa jeshi la maji la Thailand. Kama zoezi la kupiga mbizi litashindikana, kuna fursa kwamba wanaweza kuokolewa kutokea nje kwa kulichimba pango au wasubiri maji yapungue ndio watembee kwa miguu.
Lakini wakati mshale wa saa ukizidi kugonga, utabiri wa hali ya hewa unaonyesha kwamba mvua kubwa zinatarajiwa kurejea tena wiki hii mnamo ambapo msimu wa masika ukishika kasi, na hivyo kuhatarisha zoezi zima.
Kipaumbele kilichopo ni kuwapatia nguvu kabla hawajaanza zoezi la kuwaondoa. Ndugu na jamaa za wavulana hao nchini Thailand walipata ahueni baada ya kupokea taarifa za kwamba wavulana hao wako hai na salama. Timu ya uokoaji imeandaa laini za simu zilizotandazwa katika pango ili kuwapigia simu kwa mujibu wa gavana wa eneo hilo. Waokoaji walipata baiskeli, viatu vya mpira na mabegi ya mgongoni karibu na lango la kuingilia pangoni na kugundua alama za vidole na miguu zilizowaongoza kugundua mahali walikopatikana.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi /afp
Mhariri: Mohammed Khelef