1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wawakilishi wa COP28 wafikia makubaliano "ya kihistoria"

13 Desemba 2023

Wawakilishi kutoka karibu nchi 200 wamekubaliana katika mkutano wa kilele wa kimataifa wa mazingira kuanza kupunguza matumizi ya nishati ya visukuku ili kuepusha athari mbaya zaidi ya mabadiliko ya tabia nchi.

Vereinigte Arabische Emirate | COP 28 Klimakonferenz Dubai
Badhi ya wajumbe katika mkutano wa COP28, Dubai.Picha: Amr Alfiky/REUTERS

Makubaliano hayo yamefikiwa Dubai baada ya wiki mbili za vuta nikuvute katika mazungumzo yaliyolenga kupeleka ujumbe wenye nguvu kwa wawekezaji na watunga sera kwamba ulimwengu umeungana katika nia yake ya kuachana na matumizi ya nishati ya visukuku. Huu ukiwa mpango wa kwanza wa aina yake kuashiria mwisho wa enzi ya mafuta. 

Akizungumza katika mkutano huo rais wa COP28 Sultan Al Jaber ameyataja makubaliano yaliyofikiwa kama "ya kihistoria" lakini akaongeza kuwa mafanikio yake ya kweli yatakuwa katika utekelezaji wake.

"Kwa pamoja tumekabiliana na hali halisi na tumeiweka dunia katika mwelekeo sahihi, tumeweka mpango kazi thabiti ili kufikia lengo la nyuzi joto 1.5, ni mpango unaoongozwa na sayansi, ni mpango wenye usawa unaokabiliana na uzalishaji, lakini pia kuziba pengo la urekebishaji, kufikiria upya fedha za kimataifa na kuondoa hasara na uharibifu. Pia unaimarisha ushirikishwaji kamili na ushirikiano. Ni kifurushi cha kihistoria ili kuharakisha hatua ya katika suala la mazingira." amesema Al Jaber.

Soma pia: Mabadiliko ya tabia nchi ni kiticho kikubwa cha usalama wa chakula

Mpango uliafikiwa ni kwamba mataifa yanahitaji hasa "kuhama kutoka nishati ya kisukuku katika mifumo ya nishati, kwa kuzingatia haki, utaratibu na usawa ili kufikia sufuri ifikapo mwaka 2050 kwa kuzingatia sayansi.

Mapokezi ya makubaliano yaliyofikiwa

Baadhi ya wawakilishi katika mkutano wa mabadiliko ya tabia nchi huko Dubai.Picha: Amr Alfiky/Reuters

Nchi kadhaa zimeshangilia kufanikiwa kwa mpango huo, jambo ambalo halikuwezekana katika miongo kadhaa ya mazungumzo ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Soma pia: Kundi la OPEC laibua hasira kwenye mkutano wa COP28

Hata hivyo, visiwa vidogo vilivyoathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi, ambavyo vilikuwa miongoni mwa wafuasi wengi walioshinikiza kuondokana na nishati ya vusukuku kupitia Muungano wa Nchi za Visiwa Vidogo wamelalamika kuwa mpango ulioafikiwa ulikubaliwa kabla wajumbe wake hawajafika katika chumba cha mkutano na badala yake wanaukosoa wakisema kwamba lugha iliyotumika inakatisha tamaa.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen amepongeza makubaliano yaliyofikiwa kwenye mkutano wa COP28 akitaja hatua hiyo kama mapambazuko ya ulimwengu mpya usio na uhitaji wa makaa ya mawe au mafuta.

Aidha, waziri wa Mazingira wa Brazil Marina Silva amesema mataifa tajiri lazima yaongoze mabadiliko ya nishati na kuzipa nchi zinazoendelea "njia zinazohitajika" kufuata mkondo huo baada ya kupitishwa kwa mkataba wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.