Urusi na Ukraine kuanza mazungumzo ya kumaliza vita
17 Februari 2026
Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema wanacholenga ni kuzungumzia kwa upana masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na yale yaliyo muhimu zaidi. Kwenye mazungumzo hayo, vipengele vinavyogusa zaidi pande zote mbili ni pamoja na uhalali wa maeneo na kila kitu kingine kinachohusiana na masharti ambayo Urusi imekwishayatoa, aliongeza Peskov alipozungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu.
Awamu hii ya mazungumzo inafanyika Geneva siku chache kabla ya maadhimisho ya miaka minne ya vita hivyo vilivyoanza February 24, baada ya uvamizi kamili wa Urusi dhidi ya Ukraine. Maelfu wameuawa, mamilioni wengine wameyakimbia makazi yao na miji na vijiji vya Ukraine vimeharibiwa vibaya kutokana na mzozo huo.
Urusi yashinikiza kudhibiti maeneo zaidi ya Ukraine
Urusi inadhibiti karibu asilimia 20 ya eneo la taifa la Ukraine ikiwa ni pamoja na rasi ya Crimea na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Donbas mashariki mwa nchi hiyo ambayo yalichukuliwa hata kabla ya uvamizi wa 2022. Urusi aidha inaitaka Ukraine kuachilia asilimia 20 iliyosalia ya ardhi yake huko Donesk, ambayo Moscow hadi sasa imeshindwa kuikamata, suala ambalo linapingwa na Ukraine.
Hata hivyo, msemaji wa wizara ya mambo ya Nje wa Urusi Maria Zakharova amesisitiza alipozungumza na waandishi wa habari kwamba mazungumzo hayo yatazingatia maslahi ya pande zote.
Ameongeza kuwa "Siku zote tunapigania hali ya sasa kutatuliwa kwa njia za amani. Tangu 2014, tumetoa wito wa utekelezwaji wa makubaliano ya Minsk Hata baada ya 2022, tulisisitiza mara kwa mara kwamba tunaipa kipaumbele suluhu ya kisiasa na kidiplomasia, na hatujawahi kukataa kufanya mazungumzo."
Mashambulizi ya karibuni ya anga ya Urusi nchini Ukraine yameharibu miundombinu ya nishati na kuwaacha maelfu wakihangaishwa na baridi kali kutokana na kukosa umeme.
Matumaini ni madogo, Urusi ikizidi kuishambulia Ukraine
Mazungumzo haya pia yanafanyika huku kukiwa na matumaini madogo. Kulingana na Kremlin, ujumbe wa Urusi utaongozwa na msaidizi wa Rais Vladimir Putin, Vladimir Medinsky. Igor Kostyukov, mkuu wa ujasusi wa jeshi la Urusi pia atashiriki kwenye mazungumzo hayo.
Rais Donald Trump wa Marekani anayashinikiza mataifa hayo mawili kufikia makubaliano ya kuvimaliza vita hivyo vikubwa zaidi barani Ulaya tangu Vita Kuu ya Pili ya Dunia ingawa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky analalamika kwamba Trump anaishinikiza zaidi nchi yake.
Ujumbe wa Kyiv unaongozwa na Rustem Umerov, ambaye ni katibu wa Baraza la usalama wa taifa na ulinzi pamoja na mkuu wa utumishi wa rais Zelensky Kyrylo Budanov. Mjumbe maalumu wa Trump Steve Witkoff na Jared Kushner watamwakilisha kiongozi huyo wa Marekani, hii ikiwa ni kulingana na Reuters.
Lakini wakati mazungumzo hayo yakisubiriwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine Andriy Sybiga ameandika kwenye mitandao ya kijamii mapema leo kwamba Urusi inadhoofisha na kupuuza juhudi za amani baada ya kuwavurumishia mamia ya droni. Jeshi la anga la Ukraine limesema Urusi ilirusha makombora 29 na droni 396 katika mashambulizi ambayo maafisa wa eneo hilo walisema yalilenga miundombinu muhimu.