1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanachama wa CHADEMA ruksa kuchukua fomu

17 Desemba 2024

Chama kikuu cha upinzani, Chadema kimefungua dirisha kwa wanachama wake kuchukua fomu kuwania nafasi za uongozi, huku mmoja ya kigogo wake, Tundu Lissu, akiwa wa kwanza kujitwika jukumu la kuwania nafasi ya uenyekiti.

Tansania Daressalam 2024 | Führung der Oppositionspartei CHADEMA bei Treffen
Viongozi wa Chadema, kutoka kushoto Makamu Mwenyekiti Tundu Lissu, Mwenyekiti Freeman Mbowe na Katibu Mkuu John Mnyika.Picha: Eric Boniface/DW

Lissu ambaye ni makamu mwenyekiti wa ChademaTanzania Bara, anaitaja Jumanne ya leo ni siku inayoweka kumbukumbu na historia mpya kutokana na hatua yake ya kutaka kuwa kinara wa chama hicho akiwania nafasi ya uenyekiti nafasi ambayo imekuwa na historia ndefu hasa kunapotajwa vuguvugu la kisiasa ndani ya chama hicho cha upinzani.

Mwanasiasa huyo anasema dhamira ya kutaka kuleta mapinduzi ya kiutendaji ndani ya chama ndiyo kiini kikuu kilichomsukumu kujitosa katika kinyang'anyiro hicho, kauli ambayo pia aliirejea leo asubuhi wakati akizungumza na kituo kimoja cha habari

Alisema haogopi kupambana na bosi wake, Freeman Mbowe, ambaye hadi sasa bado hajaweka bayana kama yuko mbioni kutetea nafasi yake ingawa dalili kutoka kwa baadhi ya wafusai wake zinaashiria uwezekano wa kufanya hivyo.

Lissu na Mbowe wote wanamvuto mkubwa ndani ya chama chao

Iwapo Mbowe anayetajwa kuwa na uzoefu mkubwa wa siasa za chama hicho ataamua kutetea kiti chake, uwezekano wa mchuano huo kuwa wa kihistoria na pengine kutishia mustakabali wa chama chenyewe ni mkubwa.

Tundu Lissu, makamu mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani Tanzania, ChademaPicha: Emmanuel Herman/REUTERS

Wote wanatajwa kuwa na kambi zenye kuwavutia wapiga kura ndani ya chama, lakini mstari unaowatenganisha ni namna wanavyozijadili hoja zao mbele ya halaiki na hata wanapozikabili changamoto zinazoibuliwa na chama tawala CCM na serikali yake.

Ama, Lissu ameonya juu ya kile alichokiita njama za kutaka kukichafua chama hicho pamoja na mwenyekiti wake, Mbowe wakati inapowadia duru za uchaguzi akibainishwa namna alivyodokezwa mkakati uliosukwa unaotaka kuvuruga upepo wa siasa ndani ya chama hicho.

Mbali ya Lissu kujitokeza katika kinyang'anyiro hicho, kumekuwa na wagombea wengine wanaojipanga kuwania nafasi hiyo wakisema wako tayari kwa enzi mpya ndani ya chama.

Soma zaidi:Je, kuna mpasuko ndani ya Chadema?

Odero Charles Odero jina ambalo halitajwi sana katika uga wa kisiasa, ameiambia DW kuwa yuko mbioni kuchukua fomu akiamini anauwezo wa kuwashinda wapinzani wake.

Chadema imepanga kufanya mkutano wake mkuu Januari 21, siku ambayo mbivu na mbichi ndipo zitakapojulikana kuhusu nani atakuwa kinara wa chama.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW