Wawekezaji Ghuba, waendelea kufadhili nishati mbadala Afrika
19 Machi 2026
Wachambuzi waliozungumza na shirika la habari la Associated Press wameeleza kwamba pamoja na wasiwasi uliopo, zinaonekana faida kubwa tena za muda mrefu za kiuchumi kwa mataifa hayo kutokana na ufadhili huo barani Afrika na kutokana na hilo itakuwa vigumu kwa mataifa hayo ya Ghuba kuuondoa uwekezaji huo.
Ripoti iliyotolewa mwezi uliopita na Kikosi Kazi kinachoshughulikia maswala yanayohusiana na Hewa Safiimebainisha kuwa zaidi ya dola bilioni 101.9 ziliingizwaa katika sekta ya nishati mbadala barani Afrika kutoka nchi za Ghuba kufikia mwisho wa mwaka wa 2024, zikiongozwa na Umoja wa Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Qatar, Kuwait na Bahrain.
Sehemu kubwa ya uwekezaji imewekwa katika eneo la Afrika Kaskazini, Kusini mwa Afrika na katika baadhi ya sehemu kwenye nchi za Afrika Mashariki. Ni nchi za Afrika Magharibi tu ndizo zina kiwango kidogo cha ufadhili kutoka mataifa ya Ghuba.
Wawekezaji wa mataifa ya Ghuba waliotajirika kutokana na gesi na mafuta ya eneo hilo sasa wameamua kuigeukia sekta ya nishati safi barani Afrika, wakivutiwa na kuongezeka kwa mahitaji ya umeme, ukuaji wa miji kwa kasi na jukumu linaloendelea kukua barani humo katika minyororo ya usambazaji wa kimataifa inayohusiana na madini muhimu na utengenezaji bidhaa.
Wawekezaji wa mataifa ya Ghuba wageukia sekta ya nishati safi barani Afrika
Matthew Tilleard, Mkurugenzi wa kampuni ya CrossBoundary Energy, inayoendesha miradi ya nishati mbadala yenye makao yake makuu jijini Nairobi, Kenya amesema bara la Afrika linabakia kuwa moja ya maeneo machache ambako ukuaji wa mahitaji hauna shaka. Amesema kuna fursa kubwa na za muda mrefu katika miundombinu ya barani humo.
Afrika inakabiliwa na pengo kubwa la upatikanaji wa umeme wa uhakikakulingaisha na sehemu zingine duniani. Takriban watu milioni 600 kote barani humo bado hawana uwezo wa kupata umeme. Serikali za bara hilo zinawageukia wawekezaji binafsi ili kusaidia kufadhili miradi ya nishati ya jua, upepo au miradi ya umeme mseto unaochanganya vyanzo viwili au zaidi vya nishati ili kuongeza uwezo wa uzalishaji umeme bila ya matumizi makubwa ya fedha za umma. Pengo hilo linatoa fursa kwa wawekezaji wa Ghuba wanaotafuta kubadilisha uwekezaji wao kutoka kwenye mafuta na gesi.
Mkurugenzi wa kampuni ya CrossBoundary Energy, Matthew Tilleard, amesema "Kwa wawekezaji, miradi ya nishati mbadala inaweza kuwa njia mpya ya kimkakati ya kutumika viwandani itakayoweza kuipindua njia ya uzalishaji wa umeme," Tilleard amesema viiwanda vya nishati mbadala vilivyojengwa ili kusambaza migodi, au kufanya shughuli kubwa za viwanda vinawaweka wawekezaji wa Kiarabu karibu zaidi na minyororo ya usambazaji wa madini yanayotumika katika utengenezaji wa betri na katika teknolojia zingine."
Joab Okanda, mchambuzi wa maswala ya nishati na maendeleo, amesema usumbufu unaojitokeza katika usafirishaji wa mafuta na gesi kutokana na vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, vita hivyo vinanaweza kuchochea hatua za mataifa ya Ghuba kuongeza zaidi uwekezaji wao katika nishati mbadala kwani nchi hizo zimeona jinsi njia hizo za usambazaji zinavyoweza kuwa hatarini.
Louw Nelson, mchambuzi wa maswala ya siasa katika kitengo cha Uchumi kwenye chuo kikuu cha Oxford nchini Uingereza amesema "Kwa sasa kuna kiwango kikubwa cha uwekezaji wa nishati mbadalaunaoendelea kote barani Afrika, na miradi hiyo ni ya muda mrefu " Amesema uwekezaji wa nje katika sekta ya nishati mbadala ni sehemu ya mikakati mipana miongoni mwa nchi za Mashariki ya Kati zinazolenga kukuza uchumi wa mataifa hayo na pia kubadilisha namna ya uendeshaji wa shughuli za uwekezaji wan je wa mataifa hayo ya Ghuba ili kuendana na mabadiliko ya kimataifa kuelekea matumizi ya nishati safi.