1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wazambia wapiga kura katika uchaguzi wa rais

Josephat Charo
12 Agosti 2021

Wazambia wanaamua leo ikiwa wanataka kumchagua tena rais wao Edgar Lungu baada ya matokeo mabaya ya uchumi kuwahi kushuhudiwa katika miongo kadhaa na ukandamizaji dhidi ya wapinzani ambao umeibua hofu ya kuzuka machafuko

Sambia Lusaka Wahlen Frau mit Kind bei Stimmabgabe
Picha: Getty Images/AFP/G. Guercia

Raia wa Zambia wanaamua kati ya rais Edgar Lungu na mpinzani wake mkuu, Hakainde Hichilema, katika kinyang'anyiro kikali ambacho kura za maoni zinazonesha wagombea hao wakikabana koo. Hichilema mwenye umri wa miaka 59, amewahi kushindwa mara mbili na Lungu, mara ya kwanza katika uchaguzi wa 2015 baada ya kifo cha rais wa zamani Michael Sata na katika uchaguzi mkuu uliofuata mwaka mmoja baadaye.

Lungu alilituma jeshi kuzima machafuko yaliyoibuka baada ya makabiliano kati ya wafuasi wa vyama vianvyohasimiana kuelekea uchaguzi wa leo wa rais na bunge, hatua iliyokosolewa na wakosoaji kama mbinu ya kuwatisha na kuwahujumu wapigaji kura wafuasi wa upinzani. Msemaji wa chama cha rais Lungu cha Patriotic Front, PF, Antonio Mwanza, alidai siku ya Jumanne kwamba upinzani unatumia machafuko kuvuruga na kufuja mchakato wa uchaguzi na kuwatisha watu ili wasijitokeze kwa wingi kutumbukiza kura zao kwenye masanduku vituoni.

Rais Edgar Lungu anatafuta kuchaguliwa tenaPicha: Salim Dawood/AFP/Getty Images

Wachambuzi wanasema matokeo ya uchaguzi huu unaoshuhudia wagombea wakipambana kwa karibu na kukaribiana, yatatoa muelekea kwa uwekezaji katika nchi hiyo yenye utajiri wa shaba, ambako zaidi ya nusu ya wakazi wake milioni 17 wanaishi katika hali ngumu ya umasikini.

Utafiti umebainisha kuwa hali ngumu ya kiuchumi imepunguza umaarufu na uungwaji mkono wa Lungu, anayetuhumiwa kwa kuchukua mikopo mikubwa bila mpango kufadhili miradi ya kifahari ya ujenzi wa miundombinu, huku kwa upande mwingine gharama za maisha zikipanda.

Katika mji mkuu Lusaka, ilani za rangi ya kijani ya chama cha Lungu cha Patriotic Front zimechukua nafasi kubwa  kwenye mabango yaliyowekwa kando kando ya barabara mpya na madaraja ya juu. Wapigaji kura wa upinzani, ambao rangi ya chama chao ni nyekundu, wametulia bila kuonyesha hamasa kubwa katika mji huo ambao ni ngome ya chama cha Patriotic Front. Baadhi yao hata wanavaa nguo za rangi ya kijani ili kuepuka kutumbukia kwenye matatizo, katika kile kinachofahamika kama "mbinu ya matikiti maji".

Hichilema alishindwa na Lungu mara mbiliPicha: Salim Dawood/AFP/Getty Images

William Njombo, mfuasi wa chama cha upinzani cha UPND, amesema hawajihisi salama kwa kuwa kuna hali ya kutishwa sana.

Ubalozi wa Marekani mjini Lusaka umeihimiza polisi ya Zambia na jeshi kutumia sheria kwa usawa na kwa kuheshimu ubinadamu wakati wa uchaguzi wa leo. Huku machafuko yakiwa ni ya kawaida katika chaguzi za Zambia, kila mabadilishano ya madaraka yamefanyika kwa njia ya amani tangu nchi hiyo ambayo ni koloni la zamani la Uingereza iilipoanzisha siasa za vyama vingi mnamo 1990.

Hichilema na Lungu walifanya kampeni wakijinasibu kama "wanasiasa wa watu" wakiahidi ajira na utajiri kwa wapiga kura. Zaidi ya watu milioni saba wameandikishwa rasmi kupiga kura katika uchaguzi wao huku matokeo yakitarajiwa kutangazwa siku ya Jumapili. Afisa Mkuu wa tume ya uchaguzi, Patrick Nashindano, ameahidi uchaguzi utakuwa huru na wa haki. Akizungumza siku ya Jumanne Nashindano alisema tume hiyo haijishughulishi na mizengwe na uchakachuaji wa matokeo.

Matokeo ya Lusaka, mji wenye wakazi zaidi ya milioni 3.3 na mkoa wa kati wenye utajiri wa madini ya shaba, yatakuwa na umuhimu mkubwa katika kuamua mshindi. Sydney Chilong, mfanyabiashara anayeuza nguo mjini humo anasema ana matumaini watafanikiwa kuilinda amani lakini anadhani kitakuwa kipindi kigumu chenye changamoto kwao.

afp

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW