1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Wazazi wapitia wakati mgumu mjini Kherson

10 Novemba 2023

Mji wa Kherson umekumbwa na mashambulizi ya kila siku tangu ulipokombolewa tena na vikosi vya Ukraine Novemba mwaka jana na sasa wazazi wanakabiliwa na uamuzi mgumu, kuondoka na watoto wao au kubakia katika hatari.

Mama akiwa na watoto wake katika kambi moja Kherson
Mama akiwa na watoto wake katika kambi moja Kherson Picha: Hanna Sokolov/DW

Mji huo upo kwenye ukingo wa magharibi wa mto Dnipro unaodhibitiwa na Ukraine, mstari wa mbele katika uwanja wa mapambano kati ya pande mbili zinazopigana. 

Sauti za nyayo za watoto zilisikika kando ya barabara ya ukumbi wa shule katika mji wa Kherson kusini mwa Ukraine wakati wanafunzi walipokusanyika kupanda treni iliyoandikwa "Uhamishaji".

Nadiya Kondratkova alisimama akizungukwa na masanduku, midomo yake ikitetemeka na macho yake kujaa machozi. Hii ilikuwa mara yake ya kwanza kutengana na binti zake.

Nadiya amelazimika kufanya maamuzi magumu akisema lazima wanawe wapumzike mbali na milipuko na ving'ora, kwani wamechoka na wanashindwa kulala vizuri.

Wakati wanajeshi wa Ukraine walipoanzisha mashambulizi mashariki mwa mto Dnipro na mashambulizi ya Urusi kuzidi, wazazi sasa wanakabiliwa na maamuzi magumu, kukabiliana na mabomu kama familia au kuwapeleka watoto wao mahali salama.

Urusi yazidisha mashambulizi katika mji wa Ukraine wa Avdiivka

Huku hatari ikiongezeka, maafisa wa eneo hilo walianzisha mpango wa kuwahamisha watoto kwa muda hadi kwenye kambi ya likizo iliyo katika milima yenye kupendeza magharibi mwa Ukraine.

Afisa wa Kherson Anton Yefanov, akiwa amesimama karibu na basi linalojiandaa kuwahamisha watoto 65 mbali na wengine zaidi ya 280 ambao tayari wamefikishwa mahali salama amesema jukumu lao ni kuwapeleka watoto hao katika maeneo salama angalau kwa miezi kadhaa.

Watoto zaidi ya 500 wameuwawa tangu Urusi ilipoivamia Ukraine 

Jengo lililoharibiwa kwa makombora mjini KhersonPicha: Igor Burdyga/DW

Kwa mbali kunasikika vishindo vya milipuko ya mbali, huku familia za wanaohamishwa wakizungumza kwa hisia mseto  kwa vicheko na kulia.

Ukraine inasema zaidi ya watoto 500 wameuawa tangu Urusi ilipoivamia mwezi Februari mwaka jana, hatua mbaya katika mgogoro huo uliodumu kwa zaidi ya miezi 20.

Hata hivyo sio familia zote huko Kherson ziko tayari kutengana, licha ya wito wa kuhama. Volodymyr na Maryna Pchelnyk, wote wakiwa na umri wa miaka 40, walisema walipendelea kubakia pamoja na watoto wao licha ya hatari iliyopo.

Ni nadra sana kwa watoto kuonekana huko Kherson. Wanacheza kwa tiara katika eneo lililolindwa na mifuko ya mchanga au hutoka nje na wazazi wao baada ya giza kuingia, kukiwa na mashambulizi machache ya anga.

Ukraine iliandaa njia mbadala za kuwezesha kusafirisha nafaka baada ya Urusi kujiondoa kwenye makubaliano ya nafaka

Gennadiy Grytskov, mwenye umri wa miaka 43, aliamua kuikimbia Kherson mwezi uliopita, baada ya kombora kupiga  nyumba ya dadake, na kumuua mtoto wake wa kiume wa miaka 6 na pia kumjeruhi mtoto wake wa miaka 13.

Sasa anaishi kwenye eneo ambalo lilikuwa shule ya bweni huko Mykolaiv, takriban kilomita 70 kaskazini-magharibi.

Licha ya haya yote wazazi hawa wana matumaini kwamba siku moja watarudi nyumbani, kwani nyumbani ni Nyumbani.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW