Wazee Tanzania walalamika kudharauliwa huduma za afya
28 Septemba 2018Wengi ya wazee hao wanasema sera ya taifa ya mwaka 2007 inayofungua milango kwa wazee wasiojiweza kupatiwa matibabu bure haitekelezwi ipasavyo na kwamba baadhi ya waganga wafawidhi wa mikoa na hata wale wa wilaya wamekuwa wakiwatoza fedha licha ya sera hiyo kueleza bayana.
Kama hiyo haitoshi kumekuwa na ongezeko la manung’uniko KUtoka kwa wazee hao wanaosema kwamba wakati mwingine wanalazimika kuingia kwenye mifuko yao kununua dawa kwa vile hospitali nyingi zimekuwa zikidai kutokuwa na dawa za kutosha.
Ingawa serikali imeendelea kusisitiza utoaji wa matibabu bure kwa wazee wasiojiweza, hata hivyo, baadhi ya watendaji serikali kama vile wakurugenzi wa wilaya wanatajwa ndio wanaokwamisha sera hiyo.
Wengi wao wanadaiwa kutosimamia vyema mkakati huo unaowataka kuorodhesha majina ya wazee na kisha kuwapa vitambulisho ili wapatiwe matibabu bure.
Kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Waziri wa afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu; akizungumza bungeni hivi karibuni alionya juu mwenendo huo aliodai unawanyima fursa wazee kupata haki zao.
Baadhi ya wazee wanataka sera hiyo itafsiriwe kwa vitendo na kuweka mikakati bayana ya namna ya utekelezaji wake. Asilimia kubwa ya wazee hao hawana bima za afya na hivyo kuwawia vigumu kwenda katika maduka binafsi ya dawa kupata huduma wanazostahili pindi inapojitokeza dawa walizoandikiwa hazipatikani katika hospitali za serikali.
Akielezea ufumbuzi mwingine wa kukwamua changamoto zinazowakabili, mzee huyu aliyetambulika kwa jina la Abdala Nandonde anasema ni vyema serikali ikaanza kutoa malipo ya uzeeni kwa wazee wasiojiweza ili waweze kujigharimia mahitaji yao.
Ikiwa dunia imetenga Oktoba Mosi kila mwaka kama siku ya wazee, basi ni vyema kutambua kuwa siku zote uzee ni dawa.
Mwandishi: George Njogopa
Mhariri: Josephat Charo