Wazee wa Rwanda walalamikia kipato kidogo
28 Septemba 2018Mukafurere Theresa ni bibi mwenye umri wa miaka 87. Anaishi katika moja ya viunga vya mji mkuu wa Rwanda, Kigali, pamoja na baadhi ya wazee wenzake. Lakini ukimuuliza hali ya maisha yake ilivyo, ndipo unagunduwa jinsi anavyoumia.
""Siku zote mimi naumwa mwili mzima lakini kupata matibabu ni shida. Hatuna huduma ya matibabu. Mara nyingi tunaugua na kukosa matibabu. Hata chakula ni shida maana kile tunachopewa ni kama hakitoshi," anasema Bi Mukafurere anayeongeza kuwa huwa wanapatiwa mlo wa aina moja tu ambao hata maandalizi yake hayaridhishi, maana kilas siku wanakula wali na ugali wa mahindi tu.
Bi Mukafurere anawakilisha idadi kubwa ya wazee nchini Rwanda ambao hali zao za maisha haziridhishi. Wengi wanasema hawana makaazi lakini hata wachache wenye makaazi hayo, kama yeye, wanakabiliwa na changamoto kama hizo.
Wazee wenye kuhitaji msaada nchini Rwanda wako kwenye makundi mawili: wale waliowahi kuwa wafanyakazi wa serikali na ambao kwa sasa walipaswa kuwa wanapata sehemu ya pesa ya kiinua mgongo baada ya kustaafu na wale ambao ni vikongwe na ambao hakuwahi kuwa na ajira serikalini.
Makundi haya mawili yana changamoto karibu zinazofanana. Wote wamo chini ya mpango wa serikali wa kuwapatia huduma ya pesa, chakula na mahitaji mengine lakini ni kama mkakati huu bado una changamoto. Bibi Mukafurere anasema awali alikuwa akipewa kiasi kidogo cha pesa na baadaye akawa hapewi tena: "Nilipokuwa kwetu Kabuga nilikuwa napokea pesa hiyo,lakini nilipofika hapa sipati tena pesa hii, bado nahitaji msaada wa matibabu licha ya pesa."
Hata kwa wale wanaopokea msaada wa pesa, wanasema hautoshi ukiachilia mbali kwamba wakati mwingine unakawia kuwafikia.
"Tumeendelea kupaza sauti maana pesa zilikuwa kidogo japo juzi waliongeza kidogo maana ilikuwa faranga elfu tano sawa na sasa ni faranga elfu kumi na tatu.Na hata hiyo iliyongezwa ni baada ya kulia kwa muda wa miaka kumi na mitano iliyopita. Pengine ni ishara kwamba hali itaboreka baadaye maana imewekwa sheria ya kufanya marekebisho kila baada ya miaka mitano," anasema mwenyekiti wa Chama cha Wazee, Modeste Munyuzangabo.
Faranga 13,000 sawa na dola 16 za Kimarekani ndicho kiwango ambacho kisheria wangetakiwa kupatiwa wazee kwa mwezi, lakini hata hicho kidogo, wazee wanakilalamika kuwa hakifiki kwa wakati.
Kwa ujumla huu ni msaada unatolewa na serikali kupitia wizara ya serikali za mitaa. lakini kwa mujibu wa sheria hata kiasi hiki cha pesa kinatolewa kwa masharti magumu. Hii ni kwa sababu mzee anayekubaliwa kupewa msaada huo ni lazima athibitishwe kuwa hana mtoto au mtu mwingine yeyote wa kumsaidia.
Hata hivyo, serikali inasema licha ya hali kuendelea kuwa hivyo, kwa sasa wazee walau hali zao ni tofauti na hapo awali. "Angalau lakini wanaweza kusukuma maisha. Kuna tofauti ya maisha yaani kabla na baada ya kuanza kupewa msaada huu. Angalau kwa sasa wanaweza kununua chakula na sukari kidog, lakini kutokana na umri wao pesa hii haiwezi kuwa mtaji ili kuwasaidia zaidi," anasema Nyilidandi Mapambano, katibu mtendaji wa tarafa ya Kimironko jijini Kigali iliyoko chini ya wizara serikali za mitaa.