Wazimbabwe wajitayarisha kwa uchaguzi Jumatatu
29 Julai 2018Wasafiri wa kawaida waliobeba mahindi, mablanketi na sabuni za kufulia walikaa pamoja na wapiga kura wakielekea nyumbani kwa ajili ya uchaguzi wa kwanza nchini Zimbabwe tangu kiongozi aliyeongoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma Robert Mugabe kuondolewa madarakani miezi minane iliyopita.
Mabehewa sita ya treni hiyo iliondoka katika kituo kikuu cha mjini Johannesburg cha Central Park mapema jioni ya Ijumaa katika safari ya masaa 15, ya kilometa 600 katika majira haya ya baridi.
"Watu wa Zimbabwe wanahitaji maisha mapya ili waweze kusahau juu ya maisha magumu tuliyopitia chini ya yule mzee Mugabe," amesema abiria mmoja Emile Manyikunike, mwenye umri wa miaka 36, akivalia koti la baridi la ngozi lenye rangi nyeusi na fulana ya kijani yenye picha ya Bob Marley.
"Watu walikuwa wanapigwa na polisi kwa kutokubaliana na serikali, na hata hatukuweza kuwaamini majirani zetu kwasababu kila mtu wa pili alikuwa ni mpelelezi wa ZANU-PF," aliliambia shirika la habari la AFP.
Manyikunike amesema anamuunga mkono Nelson Chamisa, kiongozi kijana wa chama cha upinzani cha MDC ambaye ana matumaini ya kumshinda mshirika wa zamani na mrithi wa Mugabe, Emmerson Mnangagwa wa chama cha ZANU-PF.
Chini ya utawala wa mugabe , uchumi wa Zimbabwe uliporomoka na mamilioni walikimbilia nje ya nchi , hususan katika nchi jirani ya Afrika kusini kutafuta kazi na kukimbia utawala huo wa kikandamizaji.
"Chamisa anhitaji kuhakikisha kwamba Wazimbabwe wote wanapata ajira ili kwamba hata wale ambao wanakimbia wanaweza kurejea na kuijenga nchi yetu," manyikunike aliliambia shirika la habari la AFP.
Wazimbabwe wana shauku ya kupiga kura
"Treni hii inanipeleka nyumbani ili niweze kupiga kura na kuleta mabadiliko."
Abiria mwenzake Gertrude Tshabalala, mwenye umri wa miaka 58 , mfanyakazi wa nyumbani nchini Afrika kusini, alikuwa anaelekea nyumbani kuwatembelea wajuu zake wanne, akiwa amebeba sufuria za kupikia, vyakula vya makopo na nyama ili kuweza kusaidia uhaba wa vyakula nchini Zimbabwe.
Ana shaka iwapo Mnangagwa na ZANU-PF , chama ambacho kimeitawala nchi hiyo tangu kupata uhuru kutoka Uingereza mwaka 1980, anaweza kushindwa katika nchi ambayo imekuwa na historia ya udanganyifu katika uchaguzi.
"ZANU-PF hushinda kila mara , bila kujali chochote," alisema . "Lakini wajukuu zangu wawili ni wana umri wa kupiga kura mwaka huu na natumai tu kwamba kura zao zitaleta tija tofauti na zetu huko nyuma."
"Tunarudi nyumbani kwa kuwa tunataka nchi mpya. Ilikuwa miaka 37 na mzee yule akitawala , alikuba bahili na alitaka kila kitu kwa ajili yake tu," alisema mhudumu muuguzi, ambaye anafanyakazi mjini Johannesburg kwa miaka sita sasa.
"Nakwenda kumpigia kura kijana Chamisa. Wazee wanataka wazee wenzao. Akili zao zimezeeka, hawawezi kufikiri vizuri."
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Lilian Mtono