1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wazimbabwe wapiga kura katika uchaguzi wa kihistoria

30 Julai 2018

Wazimbabwe wanapiga kura katika uchaguzi wao wa kwanza bila jina la Robert Mugabe kuwa kwenye karatasi za kupigia kura. Ni uchaguzi ambao huenda ukaifanya nchi hiyo kutambuliwa zaidi kimataifa na kuimarisha uwekezaji

Bildkombo Simbabwe Präsidentschaftswahlen Mnangagwa Chamisa
Picha: picture-alliance/AP Photo

Karibu watu milioni 5.5 wamesajiliwa kupiga kura katika taifa hilo la Kusini mwa Afrika ambalo lina shauku kubwa ya kuona mabadiliko baada ya mkwamo wa kiuchumi na kisiasa wakati wa utawala wa karibu miongo minne wa Mugabe mwenye umri wa miaka 94. Maelfu ya waangalizi wa uchaguzi wamesambazwa kote nchini humo kuuangalia mchakato huo ambao upinzani unasema unaupendelea upande wa serikali licha ya kuhakikishiwa na tume ya uchaguzi kuwa utakuwa wa kuaminika.

Wagombea wawili wakuu ni Rais Emmerson Mnangagwa mwenye umri wa miaka 75, na ambaye alikuwa makamu wa rais aliyechukua usukani baada ya Mugabe kujiuzulu chini ya shinikizo la kijeshi mwaka jana, na Nelson Chamisa mwenye umri wa miaka 40, wakili na mhubiri ambaye alichukua uongozi wa chama kikuu cha upinzani Movevement for Democratic Change – MDC miezi michache iliyopita baada ya kifo cha kiongozi wake Morgan Tsvangirai. Tume ya uchaguzi imesema itatoa matokeo baada ya siku tano. Chamisa amepiga kura yake akisema kuwa ana uhakika wa kupata ushindi.

Zaidi ya wagombea 20 na karibu vyama vya kisiasa 130 vinashiriki katika uchaguzi huoPicha: Reuters/M. Hutchings

Zaidi ya wagombea 20 na karibu vyama vya kisiasa 130 vinashiriki katika uchaguzi huo. Kama hakuna mgombea wa urais atakayepata asilimia 50 ya kura, basi duru ya pili itaandaliwa Septemba 8. Ni uchaguzi wa kwanza kuandaliwa bila Mugabe aliyekiongoza chama cha ZANU PF kuingia madarakani katika uchaguzi wakati nchi hiyo ilipopata uhuru kutoka kwa utawala wa Waingereza mwaka wa 1980 na akaongoza kwa miaka 37. Akizungumza katika makazi yake mjini Harare jana, Mugabe alisema anatumai kuwa uchaguzi huo utaiondoa madarakani serikali isiyo ya kikatiba.

Mnangagwa alidai kuwa matamshi hayo ya Mugabe yalidhihirisha kuwa Chamisa yuko katika muungano na Mugabe. Lakini Chamisa pia alizungumza akisema hana chochote cha kuzungumzia kuhusu kauli ya Mugabe kwa sababu ana haki ya kusema chochote kama mpiga kura. Mnangagwa ambaye anatuhumiwa kwa kuhusika katika machafuko ya uchaguzi na udanganyifu chini ya Mugabe, amewaalika waangalizi wa kimataifa – ikiwemo timu ya Umoja wa Ulaya.

Josephat Charo akimhoji mwandishi wa habari Candice Mwakilyela aliyeko katika kituo cha kupiga kura Zimbabwe

This browser does not support the audio element.

Aliyekuwa rais wa Liberia Ellen Sirleaf Johnson ambaye ni kiongozi wa ujumbe wa uangalizi wa kimataifa amesema huu ni wakati muhimu sana katika safari ya demokrasia ya Zimbabwe. Uwepo wa waangalizi wa uchaguzi kutoka nchi za magharibi kwa mara ya kwanza katika miaka mingi ni kiashiria cha mazingira huru ya kisiasa, ijapokuwa wasiwasi umeibuliwa kuhusu upendeleo wa vyombo vya habari vya serikali kwa chama tawala cha Zanu PF pamoja na ukosefu wa uwazi katika uchapishaji wa karatasi za kupigia kura.

Serikali ijayo lazima ipambane na ukosefu mkubwa wa ajira na uchumi ulioharibiwa na sera iliyoungwa mkono na Mugabe ya kutwaa mashamba yaliyomilikiwa na wazungu, kuanguka kwa kilimo, kiwango kikubwa cha mfumko wa bei na kuhama kwa wawekezaji.

Mwandishi: Bruce Amani/AP/AP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga